NI historia nyingine, hiki ndicho kinachojieleza baada ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), kutangaza mkakati wa kujiimarisha kwa kuandaa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Taifa kwa ajili ya kupitisha Mapendekezo ya Marekebisho ya Katiba yake ya mwaka 1977.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977, CCM imekuwa na historia ya kujiimarisha kila mara hatua ambayo wadadisi wa kisiasa wanaiona ndiyo sababu ya kukifanya kuwa miongoni mwa vyama vikongwe imara duniani.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, katika mkutano wake na vyombo vya habari Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Dar es Salaam, ametaja moja ya sababu za marekebisho hayo ni kukiimarisha Chama.
“Juzi Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, ilikutana Chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Chamwino, jijini Dodoma kwa ajili ya kupokea taarifa kutoka kwa vitengo vya Idara za CCM ikiwa ni hatua ya kawaida ya kujiimarisha katika utendaji na uendeshaji wa shughuli za Chama,” ameeleza.
Shaka amesema Kamati Kuu ilipokea na kujadili pendekezo la kuitishwa kwa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa.
“Katika kikao cha kawaida kilichofanyika Desemba 18, mwaka jana, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa pamoja na mambo mengine ilipokea, ilijadili na kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya katiba ya CCM ya mwaka 1977,Toleo la 2020,” amesema.
MALENGO YA MAREKEBISHO YA KATIBA
Shaka ameyataja malengo ya CCM kuelekea marekebisho hayo; kuwa ni kuongeza kasi na ufanisi wa kazi za Chama na utekelezaji wa maamuzi ya vikao vya Chama.
Pia, amesema ni kukiwezesha Chama kupata viongozi imara, waadilifu na wenye uwezo mkubwa katika kuongoza na kusimamia majukumu ya Serikali za Mitaa kwa ufanisi.
Tatu, Shaka amesema ni kuongeza na kuimarisha udhibiti wa Chama kwa viongozi wake wanaochaguliwa, kuongoza na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kupitia serikali za mitaa.
Nne, amesema ni kuimarisha nguvu ya Chama katika kukabiliana na kudhibiti vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Ametaja lengo la tano, ni kuongeza uwakilishi wa Jumuia za CCM ngazi ya kata katika Mkutano Mkuu wa CCM wa Wilaya na kurekebisha itifaki ya uwakilishi unaofanana na Wenyeviti na Makatibu wa Jumuiya za CCM ngazi ya mkoa; kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na ngazi ya Wilaya, kuwa wajumbe wa mkutano Mkuu wa mkoa.
Shaka amesema kwa mujibu wa katiba ya CCM, mamlaka ya kupitisha na kurekebisha katiba ya Chama ipo mikononi mwa Mkutano Mkuu wa Taifa, chini ya Ibara ya 99(5) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, Toleo la 2020.
“Bila kuathiri uwezo wake, Mkutano Mkuu wa CCM Taifa unaweza kukiagiza kikao chochote cha CCM, kufanya kazi yoyote na Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa isipokuwa kutunga au kubadilisha sehemu yoyote ya Katiba ya Chama.
“Uchaguzi wa Wenyeviti na Makamu Makamu Mwenyekiti wa Chama,uteuzi wa mgombea wa Urais na kumthibitisha mgonbea Urais wa Zanzibar,” alinukuu.
Amesema katika kikao hicho, Kamati Kuu ya CCM Taifa imeazimia kuwasilisha kwa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, pendekezo la kuitishwa kwa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa.
RATIBA
Shaka amesema Machi 31, mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM na Halmashauri Kuu zitakutana.
Amesema Aprili Mosi, mwaka huu, utafanyika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa, ambapo vikao vyote vilivyotajwa vitafanyika Makao Makuu ya CCM, Dodoma.
Shaka amesema CCM imekuwa na utaratibu wa kujiimarisha nyakati zote tangu mwaka 1977 baada ya kuundwa kwake kwa vipindi tofauti imekuwa na utaratibu huo.
Alisema mwaka 1992 baada ya mfumo wa vyama vingi kurasimishwa nchini, CCM ilijitathmini na kujipanga na kujiimarisha upya kimuundo, kiutendaji,kiuchumi, kijamii na kimwelekeo ili kutoa fursa ya kukidhi nyakati zilizopo.
UCHAGUZI WA CCM
“ Mabadiliko haya ya Katiba ya CCM ni sehemu ya kujiimarisha na kama tunavyosema tunaelekea kwenye uchaguzi, yapo maeneo ambayo kama Chama tumehisi hatujafanya vizuri, maeneo hayo tunakwenda kujiimarisha.
“ Ni kweli makatibu wa mikoa walikuwa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM lakini ikaja katikati makatibu hao wakatoka ,sasa makatibu hao wanarudi kwa sababu ya kuimarisha nguvu za Chama na tathmini ya vikao vya Chama imeona Makatibu wanapaswa kuwa sehemu ya wajunmbe wa Halmashauri Kuu ya CCM,” amefafanua.
Amesema jambo la marekebisho hayo si geni, bali linaendana na matarajio ya nyakati zilizopo na kujiimarisha, huko ndipo kulipoipa fursa CCM ya kuendelea kuaminiwa kwa kupata ridhaa katika chaguzi mbalimbali kwa sababu Chama huwa kinajitathmini na kuchukua hatua ya kujiimarisha zaidi.
Shaka ameeleza kuwa, CCM tangu kuundwa kinaishi katika misingi yake na mkuu ukiwa ni katiba, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa nyakati zote.
“Ndiyo maana tunaona kila kukicha inazidi kuimarika na inapofika wakati wa uchaguzi nafasi zote za kugombea zinakuwa katika ngazi husika ya Chama na hazuiwi mwanachama yeyote kuomba ridhaa nafasi yeyote ndani ya Chama,” alieleza.
Amesema kila mwanachama mwenye sifa, anayo haki ya kugombea nafasi yoyote ndani ya Chama.
Shaka amewataka wanachama wote wa CCM kutumia fursa ya kikatiba kuomba ridhaa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Hata hivyo, amesema katika uchaguzi huo, CCM itaendelea kuwa kinara wa kupinga rushwa na wataufuatilia uchaguzi huo na mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa atachukuliwa hatua stahiki.
CCM ilizaliwa Februari 5, 1977 baada ya kuunganishwa Vyama vya ukombozi vya TANU na ASP.
Na ATHNATH MKIRAMWENI