NAKALA ya kwanza ya gazeti la UHURU ilitoka katika mtambo wa uchapaji Desemba 9 mwaka 1961, siku Tanganyika ilipopata Uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza.
Hivyo leo gazeti hili limetimiza umri wa miaka 60. Liliwapika waandishi na wahariri mahiri nchini. Siyo wanahabari tu, UHURU pia limetoa hadi viongozi wakubwa wa kisiasa, akiwemo hayati Rais Benjamin Mkapa.
Miaka 60 siyo umri mdogo. Kama ni mtu amekwishafikia uzee na anastaafu anastaafu kufanya kazi. Lakini kama gazeti, ambalo ni chombo cha habari, siyo kama limezeeka, bali limekomaa na linatakiwa liendelee kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha, lakini na kwa sasa kuna nguzo nyingine ya kazi za chombo cha habari, nayo ni kufanya biashara na kutengeneza pesa.
Gazeti lilipitia vipindi vitatu vikubwa tofauti lakini vyote ni endelevu na mtambuka: Kwanza, harakati za kupigania uhuru na kuunga mkono ukombozi wa Afrika (kabla ya uhuru na miaka ya mwanzo ya 1960 na hata baadaye mpaka Afrika Kusini ikakombolewa baada ya kung’olewa kwa utawala wa makaburu, mwaka 1994).
Pili, kujenga taifa na kuleta maendeleo (Azimio la Arusha, 1967, Operesheni Vijiji, 1974, Mipango ya Maendeleo ya Miaka Mitano, n.k.) Tatu, ulegezaji wa masharti ya uchumi na siasa nchini uliosababisha pamoja na mambo mengine, mashindano ya kupashana habari, kuchipuka kwa magazeti na vyombo vya habari vingi nchini na mitandao ya kijamii na kurejeshwa upya kwa mfumo wa vyama vingi na kuendeleza sekta binafsi.
Na kila kipindi katika hivyo vitatu, kulikuwa na mkazo maalumu katika sera za uhariri.
Likiwa gazeti kamili, UHURU lilianza kuwa la kila wiki, likitolewa kila Jumamosi na chama cha siasa kilicholeta Uhuru wa Tanganyika, TANU (Tanganyika African National Union).
Chama hicho kiliungana na ASP (Afro-Shiraz Party) kilicholeta Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoung’oa kwa nguvu utawala wa kisultani uliokuwa unaungwa mkono na wakoloni wa Kiingereza, na kuzaliwa kwa CCM (Chama Cha Mapinduzi), Februari 5, 1977.
Tanganyika nayo iliungana na Zanzibar, Aprili 26, 1964 na kuunda hii Tanzania ya sasa. Kabla ya gazeti hilo, lililokuwa linachapwa na The Dar es Salaam Printers, TANU ilikuwa na kijarida kilichokuwa kinatolewa mara kwa mara, kuelezea habari mbalimbali, hasa za kisiasa na kutangaza kwa umma maazimio ya Halmashauri Kuu ya TANU, kupitia idara yake ndogo ya kupiga chapa,
TANU Press. UHURU siyo gazeti la kwanza la Kiswahili nchini. Gazeti la kwanza la Kiswahili ni Msimulizi lililotoka karne ya 19, mwaka 1888, na kuchapishwa na kutolewa Zanzibar na taasisi ya kidini ya UMCA (Anglican Universities’ Mission), kwa mujibu wa utafiti wa Martin Sturmer (1998) wa historia ya vyombo vya habari nchini.
Msimulizi lilifuatiwa miaka mitatu baadaye, 1891, na jingine la Kiswahili, Mtenga Watu, nalo lililochapishwa na UMCA, lakini Tanzania Bara.
UHURU lilipitia mabadiliko mbalimbali hasa ya kimuundo na kiutendaji. Wakati gazeti linaanza, lilikuwa linatolewa moja kwa moja na TANU, chini ya wadhamini: Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere; Makamu wa Rais, Rashid Kawawa; Katibu Mkuu, Oscar Kambona na Sheikh Amri Abeid, ambaye alitambuliwa wakati huo kuwa Mwanachama wa Halmashauri ya Ofisi Kuu.
Mhariri, au wakati huo akiitwa Mtengenezaji, ni Kaminyoge Roland Mwanjisi. Baadaye ikaanzishwa kampuni ya TANU, Mwananchi Publishing Ltd., kusimamia uchapishaji na uchapaji wa gazeti. Mwaka 1964, likaanzishwa gazeti la TANU la Kiingereza.
Ni gazeti la The Nationalist, lililokuwa mstari wa mbele kupambana na propaganda za magazeti yaliyokuwa yanachapishwa kwa lugha ya Kiingereza ya ndani ya nchi, jirani Afrika Mashariki na kwigineko, hasa katika suala la uhuru kutoka kwa wakoloni na ukombozi wa Afrika. Baada ya Roland Mwanjisi, Mhariri Mtendaji aliyefuata ni Joel Mgogo.
Lakini mwaka 1966 yakatokea mabadiliko mengine makubwa ya muundo na Kampuni hiyo ya TANU ikabadilishwa na kuwa Mwananchi Publishing (1966) Company Ltd, na Mhariri Mtendaji akawa, Benjamin Mkapa.
Kampuni hiyo ikajikita katika shughuli za uchapishaji wa gazeti na kwamba shughuli za uchapaji zikapelekwa kwa kampuni nyingine iliyoanzishwa na serikali wakati huo chini ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Kampuni ya Uchapaji ya Taifa – KIUTA (National Printing Company – NPC).
Kampuni zote mbili, zikaendelea kuwa katika kiwanja kimoja, Barabara ya Nyerere na kushirikiana majengo.
Mabadiliko mengine yakaja mwaka 1972 wakati gazeti la TANU la Kiingereza The Nationalist, lilipounganishwa na gazeti la Kiingereza lililokuwa linatolewa na kampuni binafsi lililotaifishwa, The Standard na kuzaliwa gazeti la sasa la serikali la Kiingereza, The Daily News.
Hivyo, Ferdinand Ruhinda, mwanahabari nguli aliyekuwa Radio Tanzania na kuhamia UHURU mwaka 1966, akawa Mhariri Mtendaji mpya wa UHURU na Mkapa akapelekwa The Daily News.
Mabadiliko hayakuishia hapo, Kampuni hiyo ya TANU ikabadilishwa tena na kuwa Shirika la Magazeti ya Chama na baadaye UHURU Publications Ltd. (UPL) na uongozi kubadilishwa badilishwa na wakati fulani mtendaji mkuu wa kampuni akawa Mkurugenzi Mtendaji badala ya Mhariri Mtendaji.
(Waliowahi kushika nafasi hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji, baada ya kampuni kuongeza shughuli zake na kuwa tena na shughuli ya uchapaji ilipopata mtambo wake wa kuchapia, mwaka 1995, ni Ali Ameir Mohammed, aliyepata pia kuwa Mhariri Mtendaji hapo awali, Daniel Ole Njoolay na Adam Ngamilo).
Mwaka 2000 yakatokea mabadiliko mengine na kurudisha muundo wa mkuu wa kampuni kuwa tena Mhariri Mtendaji na kufutwa kwa cheo cha Mkurugenzi Mtendaji, baada ya utafiti uliofanywa na wataalamu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuhusu kuiimarisha UPL kibiashara.
Saidi Nguba, aliyekuwa Mhariri Mkuu wa UHURU wakati huo tangu mwaka 1997, akateuliwa kuwa Mhariri Mtendaji katika muundo huo uliorudishwa upya.
Wengine waliopata kuwa Wahariri Wakuu na Watendaji wa UHURU, ambalo likawa na gazeti dada la kila wiki, MZALENDO, lililoanzishwa mwaka 1972, na baadaye la starehe BURUDANI la kila wiki, baada ya Ruhinda, ni Costa Kumalija, Wilson Bhukoli, Ali Ameir Mohammed, Yahya Buzaragi na Josiah Mufungo.
Mabadiliko ya hivi karibuni ni kuanzishwa kwa UHURU Media Group, ingawa mchakato wa kukamilisha rasmi mfumo huo umekuwa ukiendelea. Chini ya UHURU Media Group, mtendaji mkuu anakuwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu ambaye atasimamia UPL (magazeti, yatakayokuwa chini ya Mhariri Mtendaji); People’s Media (Radio UHURU FM) na Channel 10 (Televisheni).
UHURU imeendelea kuishi, licha ya sasa kuwepo kwa magazeti na machapisho yapatayo 270; vituo vya redio za mtandaoni 20 na televisheni za mtandao 500, kwa mujibu wa Waziri wa Habari na Mawasiliano, Dk. Ashatu Kijaji hivi karibuni.
Lakini je, UHURU inatimiza malengo ya kuanzishwa kwake? Mdhamini wa gazeti la UHURU na aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Wakurugenzi ya gazeti hilo, Rashidi Kawawa, katika risala yake ya kulitakia heri gazeti la UHURU, iliyochapishwa katika nakala ya kwanza, alisema wananchi wanahitaji kuambiwa ukweli wa mambo mbalimbali yanayotendeka katika nchi yao na katika dunia nzima.
“Kuna mambo mengi sana ya maana kwa taifa letu yanayotendeka katika nchi hii, lakini hayatangazwi sawa sawa na kwa hivyo yanapotea bure. “Gazeti letu la UHURU litasaidia kuondoa shida hii…” Mzee Kawawa alisema.
Kwa kiwango gani lengo hilo limefikiwa ni suala la mjadala.
Lakini ili kufikia “wananchi wetu…kuambiwa ukweli wa mambo mbalimbali yanayotendeka katika nchi yao na katika dunia nzima,” kama alivyosema Mzee Kawawa, lazima gazeti hilo lisimame kwenye ukweli na liaminike kwa wasomaji wake.
Kama halitatoa habari za kweli na kujikita katika taaluma na weledi, bila ya woga, basi siyo wananchi tu, bali hata wanachama wa chama kinachomiliki gazeti hilo, hawatalisoma kwa sababu hawataliamini.
Hivyo gazeti lisikubali kuwa mwangi wa matamshi ya wanasiasa wenye hila na wanaowazuga watu, ili waendelee kuchaguliwa na kubaki madarakani daima dumu, bali liwe linaandika habari za ukweli na bila ya woga ili kutimiza wajibu wake na watu waliamini.
Ili kutimiza wajibu huo wa gazeti ni vema maofisa watendaji wa Chama, kinachomiliki gazeti hilo, wasiingilie utendaji wa kihariri wa gazeti ili weledi uzingatiwe na gazeti liaminike.
Maofisa watendaji wa chama, au wanasiasa wafanye kazi zao na wahariri na wanahabari nao waachwe kufanya kazi zao. Ikifika mahali mtendaji wa chama, anaingilia kati na kuamua habari ipi ichapishwe ukurasa wa kwanza na ipi iwekwe ndani, basi hata hayo aliyoyasema Kawawa ya “wananchi kuambiwa ukweli wa mambo yanayotendeka katika nchi yao na katika dunia nzima” hayatafikiwa.
Kama watendaji hao wa chama wana uwezo wa kuendesha gazeti kitaaluma, sasa wataalamu kama Mhariri na Waandishi wa Habari wanaajiriwa kufanya nini? Haya ya weledi na uhuru wa habari, yamo katika chapisho la Maadili ya Waandishi wa Habari wa Shirika la Magazeti ya Chama la mwaka 1992 na Mwongozo wa Uandishi wa Habari katika magazeti hayo, uliotolewa mwaka huo huo na shirika hilo.
Katika sehemu inayohusu uhuru wa vyombo vya habari, mwogozo huo wa Shirika la Magazeti ya Chama unasema: “Waandishi wa Habari wa Magazeti ya Chama, kama waandishi wengine, wanao uhuru wa kuandika habari zote za matukio muhimu ndani na nje ya jamii yetu.
Wanao uhuru pia wa kufichua madhambi mbalimbali katika vyombo vya utekelezaji ikiwemo wizi, ubadhirifu, uonevu na kutowajibika…”. Ni ukweli kwa wakati huo na ukweli zaidi kwa sasa.
Miongoni mwa mafanikio na maendeleo makubwa ya UHURU ni, kwanza, kuendelea kuwepo kwa gazeti lenyewe hadi katika kipindi hiki cha mashindano makubwa ya vyombo vya habari nchini, hasa ujio wa vyombo vingi, ikiwa ni pamoja na vile vya kwenye mitandao.
Pili, kuanzishwa kwa Radio UHURU, sasa UHURU FM, kwa kushirikiana na wafanyabiashara wakereketwa wa CCM. Tatu, kurejea tena kuwa na mtambo wake wa kuchapia, chini ya kampuni yake tanzu ya Modern Newspaper Printers (MNP), kuanzia mwaka 1995, ili kupunguza matatizo ya uchapaji na kumudu gharama kubwa za uchapaji na kuwa kitega uchumi.
Ingawa jambo hili halikudumu sana. MNP ilikufa mwaka 2013 na mtambo ukauzwa kutokana na uchakavu.
Ni vizuri ikumbukwe kuwa UHURU ilikuwa na mtambo wake mkubwa wa kuchapa, Goss Community, ambao ulikuwa ni msaada kutoka Ujerumani mwaka 1963.
Lakini mtambo huo, ukaachiwa Kiuta katika mabadiliko ya mfumo wa utendaji wa Mwananchi Publishing Company, mwaka 1966. Mafanikio mengine ni UHURU pia kuwa gazeti la kwanza nchini linalochapishwa kwa Kiswahili kuanza kuchapwa kwa rangi, mwaka 1997, na magazeti mengine kufuata baadaye.
Gazeti la kwanza kuchapwa kwa rangi nchini lilikuwa ni la Kiingereza, The Express, lililokuwa linatolewa na kampuni binafsi ambalo, hata hivyo lilikuwa linachapiwa Nairobi.
UHURU pia inabidi, labda chini ya mfumo mpya wa UHURU Media Group, kuwa kwanza, na mtambo wake mpya wa kisasa wa uchapaji kupunguza matatizo ya uchapaji na kuwa kitega uchumi.
Pili, kuwa na jengo lake kubwa la makao makuu, ili ofisi zake ziwe humo, na kufanya biashara ya kupangisha,ili kuwa na kitega uchumi kingine.
Lakini pia inabidi kuimarisha Radio na Televisheni kwa sharti kuwa vyombo vyote hivyo viendeshwe kibiashara na kitaaluma vikiwa na wanataaluma waliobobea, tena kwa weledi mkubwa.
Siyo busara kamwe kubeza mafanikio yaliyopatikana nchini tangu uhuru katika kujiletea maendeleo na hasa kukabiliana na maadui watatu wakubwa: Umasikini, Ujinga na Maradhi.
Lakini pia lazima tukiri kuwa kuna upungufu uliotokea katika utekelezaji wa mikakati ya kupambana na maadui hao. Ndiyo maana malengo hayajafikiwa vizuri. Umasikini bado changamoto, Ujinga hatujauondoa moja kwa moja na Maradhi bado tunapambana nayo.
UHURU imeyashuhudia hayo yote na imeendelea kuwahabarisha wananchi juu ya harakati hizo za maendeleo na upungufu katika utekelezaji wake. Iendelee kufanya hivyo, madhali bado ipo.
Ni matumaini ya wengi kwamba UHURU, kama vyombo vingine vya habari, itaendelea na majukumu yake kwa uadilifu, weledi na umahiri mkubwa katika kuendelea kutoa mchango wake katika harakati za kuleta maendeleo ya nchi kama wazee wetu waanzilishi wake walivyokuwa wanalenga.
Watakaokuwepo miaka 100 ya gazeti la UHURU au miaka mingine 60 ijayo, itabidi washuhudie hatua kubwa zaidi ya maendeleo.
- Mwandishi wa Makala hii alikuwa Mhariri Mkuu (1997 – 2000) na Mhariri Mtendaji (2000 – 2004) wa Gazeti la UHURU. Alikuwa pia Mhariri Mtendaji wa Gazeti la MWANANCHI (2004 – 2005). Baadaye alikuwa Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu (2006 – 2013). Hivi sasa ni Mshauri wa masuala ya Habari, Mawasiliano na Mahusiano chini ya Kampuni ya Pioneer Communications nchini. Anapatikana kwa Simu ya Kiganjani/WhatsApp: 0754-388418 na Barua-pepe: sanguba@gmail.com