BENKI ya NMB imekabidhi vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. Milioni 12 kwa timu ya Bunge Sports Club kwa ajili ya kushiriki tamasha litakalofanyika septemba 4, 2021 katika viwanja vya jamhuri na Chinangali Park.
Akizungumza jijini humo kabla ya kukabidhi vifaa hivyo Afisa Mkuu wa Fedha NMB, Juma Kimori, amesema tamasha hilo litahusisha michezo saba ambayo itakutanisha wabunge na wafanyakazi wa NMB.
Ameeleza michezo hiyo ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa kikapu wanaume na wanawake, mpira wa wavu, mpira pete, Kuvuta kamba na kukimbiza kuku.
“Sisi kama NMB tunatambua mchango wenu mkubwa katika kutunga sheria mbalimbali pamoja na wajibu wa kuisimamia serikali muwapo ndani na nje ya bunge
lakini pia michezo inatuunganisha watu wote na hivyo michezo hii itakuwa chachu kubwa ya kujenga umoja na mahusiano mazuri ya nje ya bunge baada ya kazi kubwa mnayoendelea kuifanya katika kipindi hiki,”amesema.
Mwenyekiti wa Bunge ‘Sports Club’, Abbas Tarimba amesema timu ya bunge imejiandaa kutoa kichapo kwa timu ya benki hiyo huku akitahadharisha kutowekewa wachezaji mamluki (wasio ndani ya benki)
Pia, Tarimba ametumia nafasi hiyo kuipongeza na kuishukuru benki hiyo kwa kutoa vifaa hivyo na kuahidi ushirikiano zaidi kwa benki hiyo.
Na SELINA MATHEW, Dodoma