HATIMAYE michuano ya UEFA EURO 2020, imefika hatua ya nusu fainali, ambapo leo nyasi za uwanja wa Wembley,nchini Uingereza, zinatarajiwa kuwaka moto zitakapoipokea mechi ya kwanza ya hatua hiyo kati ya Italia na Hispania.
Kadhalika, uwanja huo ndio utakaohudumia mechi ya pili ya nusu fainali kati ya wenyeji Uingereza na Denmark, Julai 6, mwaka huu.
ITALIA Vs HISPANIA
Kihistoria, Italia imeshinda taji hilo la EURO mara moja mwaka 1968 na Hispania imelibeba mara tatu yaani mwaka 1964, 2008 na 2012.
Timu hizo katika michuano hiyo ya Ulaya na Kombe la Dunia zimekutana mara tisa,Italia ikishinda mara nne dhidi ya mara moja ya Hispania na zikatoka suluhu mara nne.
UINGEREZA Vs DENMARK
Kesho Julai 7, Uingereza nayo itakuwa na kibarua cha nusu fainali ya pili dhidi ya wabishi Denmark, mchezo utakaokuwa wa tatu kwa mataifa hayo kukutana katika michuano mikubwa ya kimataifa.
Katika mikutano hiyo, Denmark ilianza kumnyanyasa Muingereza kwa ushindi katika hatua ya makundi ya EURO 1992 na baadaye Uingereza ilirudisha kisasi katika mzunguko wa pili wa Kombe la Dunia 2002 kwa kushinda goli 3-0.
Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa Uingereza ina matumaini ya kufika katika fainali ya michuano hiyo, baada ya kushindwa kupata mafanikio kama hayo tangu iliponyakua kombe la dunia mwaka 1966.
Mwaka 1996 Uingereza pia ilifika katika hatua hiyo ya nusu fainali na baadaye matokeo mazuri iliyapata mwaka 1968 ilipomaliza katika nafasi ya tatu.
Kwa upande wa Denmark, nayo inajitosa katka vita hiyo na Waingereza ikiwa na kumbukumbu ya kuingia nusu fainali ya EURO mwaka 1984 na baadaye mwaka 1992 ilitwaa taji hilo.
Na William Shechambo kwa msaada wa intaneti