Na BALTAZAR MASHAKA, MAGU
OFISA Elimu, Mhandisi na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabila, Wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, wamekalia kuti ‘kavu’, baada ya mradi wa bweni la shule hiyo kushindwa kukamilika kwa wakati.
Hayo yalijiri juzi, baada ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde, kutembelea mradi huo na kuagiza bweni hilo liwe likamilika ifikapo Mei, mwaka huu.
Silinde, alitishia kuwavua madaraka watendaji hao endapo watashindwa kukamilisha ujenzi huo, huku akiwataka waandike barua TAMISEMI wajieleze kwa nini ujenzi huo umechelewa kukamilika.
“Naagiza ujenzi wa bweni hilo ifikapo Mei, mwaka huu, uwe umekamilika na nitakuja kukagua jengo hilo. Ofisa Elimu wa Wilaya, Mhandisi wa Wilaya na Mkuu wa Shule, naagiza waandike barua TAMISEMI, wajieleze kwa nini ujenzi huo umechelewa kukamilika na wakishindwa kulikamilisha, nitawavua madaraka yao,” alisema Silinde.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Simon Mpandalume, alisema kutokana na maagizo ya Naibu Waziri, aliiomba serikali wilaya ya Magu, kumhoji Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabila, Edgar Kalokola, kuhusu tuhuma za matumizi mabaya na usimamizi mbovu wa fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo.
Alisema ujenzi huo bado unasusua huku fedha zote za mradi, ambazo ni sh. milioni 80, zikiwa zimeshatolewa huku jengo halijakamilika.
“Wakati halmashauri tukikamilisha ujenzi huo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani, ipo haja ya kuwaita wote wanaohusika na usimamizi wa jengo hilo ili kuhojiwa,” alisisitiza.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kabila, Kalokola, alisema kilichosababisha ujenzi huo kuchelewa ni umbali wa upatikanaji wa malighafi za ujenzi, hivyo kusababisha gharama za ujenzi kuongezeka.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Silinde, aliwaagiza wakuu wa shule za Buhongwa, Kwimba, Buswelu na Ilemela, kundika barua kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu, ikiwemo kuvuliwa madaraka yao kwa kuchelewesha ujenzi wa mabweni kwenye shule zao.