MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, amewataka Watanzania kutumia vizuri uwepo wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, kwani ni fursa muhimu ya kujenga misingi imara ya maridhiano na umoja wa kitaifa.
Amesema anamwelewa Rais Samia kutokana na maono yenye tija aliyonayo kwa maendeleo ya taifa na uwepo wake ni fursa ya pekee.
Akizungumza katika kituo cha Televisheni cha Clouds kupitia kipindi cha Clouds 360, Masoud, alisema moja ya mambo ambayo Rais Samia aliyoacha historia Zanzibar mwaka 2014, ni kufanya mabadiliko katika mfumo wa sheria za kazi.
“Namwelewa kwa uchapakazi wake, maono yake na kutoweka vizingiti kwa mtu, kwa Tanzania ilipo sasa kama kuna wakati wa kutumia vizuri nafasi yetu ni sasa, kwa sababu dunia yenyewe inabadilika sana, unaweza kuwadhibiti watu kwa mifumo mizuri,” alisema.
Aidha, Masoud alisema Rais Samia alisimamia vizuri mabadiliko ya sheria za kazi na alionyesha umahiri kwa kuja na sheria mpya saba.
Akizungumza kuhusu katiba mpya, Masoud alishauri mchakato wake usihusishwe na itikadi za kisiasa.
”Tunapokwenda katika katiba mpya tuache kufikiria vyama, kwamba chama fulani kitanufaika, hayo sio mambo ya kufikiria sasa,” alisema.
UCHUMI WA BULUU
Aidha, Masoud alisema uchumi wa buluu ni eneo bora la kuwekeza na sasa serikali inatazama ni kiasi gani unatumika kuleta manufaa ya kiuchumi.
Aliongeza kupitia uchumi wa buluu, wananchi wameanza kupata mwamko wa uvuvi mkubwa na kuondoa mawazo ya kuendelea kujihusisha na uvuvi mdogo.
KUHUSU MUUNGANO
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, akizungumzia Muungano, alisema unapaswa kutazamwa katika mtazamo mpana ikiwemo kuzingatia misingi ya kiuchumi ili kuleta manufaa zaidi.
“Hatujafika mahali tukautazama Muungano katika misingi ya uchumi, tungekuwa tunaangalia nini mchango wa Zanzibar katika mchango wa Jamhuri na kushirikiana vipi na Tanzania Bara katika misingi ya uchumi,” alisema.
HAYATI MAALIM SEIF
Akimzungumzia aliyekuwa mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, alisema ataendelea kumuenzi kwa kuhakikisha anawaunganisha Wazanzibari.
Alisema Maalim Seif alikuwa mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa, hivyo atahakikisha anaziishi dhamira zake.
Na IRENE MWASOMOLA