KOCHA wa Simba, Pablo Franco, amesema kikosi chake kitavuna pointi tatu katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC itakayochezwa kesho.
Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 18, katika mechi nane ilizocheza, itakuwa ugenini kuikabili KMC kesho, saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.
Wekundu hao wa Msimbazi watashuka dimbani ikiwa ni siku chache baada ya kushindwa kucheza pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, katika mechi iliyopangwa kufanyika Desemba 18, mwaka huu mjini Bukoba, baada ya kuthibitika kuwa, asilimia kubwa ya wachezaji wake walikuwa wagonjwa.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, watashuka dimbani wakiwa chini ya uangalizi wa madaktari na wataalamu wa afya ili kutoa huduma ya haraka iwapo kutakuwa na wagonjwa wengine wanaosumbuliwa na mafua makali yaliowakumba wachezaji wa timu hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Pablo alisema kikosi chake kimejipanga vyema kimbinu na kiufundi ili kupata ushindi katika mechi hiyo.
Alisema anajua mchezo huo utakuwa mgumu kwani timu yake inapocheza ugenini hukabiliwa na upinzani mkali.
“Wachezaji wanaendelea vizuri na wapo chini ya uangalizi wa madakatari wetu, huu mchezo ni muhimu kwetu na ninaamini watapambana na kuvuna pointi ambazo zitazidi kutuweka katika nafasi nzuri,” alisema Pablo.
Nahodha Msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, alisema timu imefika salama mjini Tabora na ilitarajia kufanya mazoezi mepesi ya kujiweka sawa (jana jioni) tayari kuwakabili wapinzani wao.
Tshabalala alisema ana uhakika watafanya vizuri pamoja na kucheza ugenini huku akiwa na uhakika kuwa kikosi chake kimekamiwa.
MORRISON NJE
Wakati Simba ikijiwinda na mtanange huo, Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ali Shatry ‘Chiko’, alisema Simba itawamkosa Bernard Morrison na Tadeo Lwanga.
Chiko alisema, afya ya Morrison bado haijaimarika wakati Lwanga anaendelea kuuguza jeraha la goti.
Simba ilianza ligi kwa suluhu dhidi ya Biashara United kisha ikashinda bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji na kuichapa bao 1-0 Polisi Tanzania kabla ya suluhu dhidi ya Coastal Union na ushindi wa bao 1-0 ilipocheza na Namungo FC wakati iliichapa mabao 3-1 Ruvu Shooting, ilishinda mabao 2-1 ilipocheza na Geita Gold kabla ya suluhu ilipokutana na Yanga.
Na NASRA KITANA