BAADA ya kuanza vyema katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting, kwa kuichapa mabao 3-1, Kocha wa Simba, Pablo Franco raia wa Hispania, amepewa mitihani miwili ndani ya klabu hiyo.
Uongozi wa Klabu ya Simba, umempa kocha huyo mtihani wa kwanza kuhakikisha anaifikisha timu katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na mtihani wa pili ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara walioutwaa mara nne mfululizo.
Akizungumza Dar es Salaam, katika mkutano wa klabu hiyo uliofanyika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez, alisema kipaumbele cha kwanza ambacho wamempa Kocha Pablo ni kuhakikisha wanatinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho na kutetea taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Barbara alisema licha ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika, ila bado wanahitaji kufanya vizuri katika michuano hiyo katika msimu huu.
“Malengo yetu msimu huu ilikuwa ni kutetea ubingwa, kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa lakini tumeteleza, hivyo Mwenyezi Mungu ametupa nafasi nyingine katika Kombe la Shirikisho, kocha tunaye na naamini tutafikia tunapopataka,” alisema Barbara.
Aidha, Barbara alimpongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo’, kwa mafanikio waliyoyapata chini ya uongozi wake kwa kushinda mara nne mataji ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
MO APEWA URAS SIMBA
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alimtangaza Mwekezaji wa klabu hiyo Mohamed Dewji ‘Mo’ kuwa rais wa heshima ndani ya Simba kutokana na mambo mazuri anayoendelea kuyafanya.
Try Again alisema Simba imempa heshima hiyo Mo kutokana na mchango wake mkubwa alioufanya na anaoendelea kuufanya ndani ya klabu ya Simba.
“Kwa kutambua mchango wake mkubwa na makubwa aliyotufanyia katika klabu hii, kwa mapenzi ya dhati, katika kikao cha bodi kilichokaa hivi karibuni, bodi imeamua kumpa urais wa heshima Mo,” alisema Try Again.
Hata hivyo, aliongeza mabadiliko yamekamilika na mwekezaji Mo ameshaweka sh. bilioni 20 na watapata sh. milioni 200 kila mwezi kwa ajili ya shughuli za klabu.
Wakati huo huo aliyekuwa mchezaji wa Simba kwa sasa anakipigia Berkane ya Morocco, Clatous Chama alisimamisha kwa muda hotuba ya ‘Try Again’ katika mkutano mkuu wa klabu hiyo baada ya kutajwa jina lake.
Wanachama walilipuka kwa furaha wakati Try Again alipowaeleza kwamba wana uwezo wa kumsajili mchezaji yoyote wanayemtaka baada ya mwekezaji wa klabu hiyo, Mo kumhakikishia fedha zipo.
“Tutamleta yeyote katika usajili, sijui awe Chama au nani, kwani Mo ametuhakikishia kuwa hela ya kufanya usajili ipo yakutosha,” alisema Try Again Baada ya kauli hiyo, wajumbe waliohudhuria katika mkutano huo, walilipuka kwa shangwe wakiamini ni taarifa nzuri kwao.
Hali hiyo iliyosababisha Try Again kusimama kwa sekunde chache kusubiri wanachama wamalize kushangilia na baadaye aliendelea na hotuba yake.
KASSIM DEWJI AMRITH HANS POPPE
Mwenyekiti wa bodi Try Again alimtangaza Kassim Dewji kuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo.
Dewji anachukua nafasi ya Zacharia Hans Poppe aliyefariki Septemba mwaka huu na kuzikwa mkoani Iringa.
“Tunafahamu uwezo Dewji, hivyo bodi imemkabidhi jukumu la kuongoza kamati ya usajili ambayo ilikuwa chini ya Hans Poppe enzi za uhai wake,” alisema Try Again
ZUNGU AFUNGUKA
Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azzan Zungu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alisema mpira una gharama na gharama za mpira sio uwekezaji wa pesa bali ni kupata machungu ya kufungwa.
“Tusitegemee kuwa timu yetu haitafungwa, kuna mambo mengi yanayofanya timu ifungwe, kuna mambo ya makusudi, uzembe lakini kuna kuzidiwa na muda mwingine wachezaji kuchoka kwa hiyo tushinde pamoja na tufungwe pamoja sio tukishinda uongozi mzuri na tukifungwa viongozi wabaya, tujue kuwa viongozi ndio wanatusaidia,” alisema.
Hata hivyo Zungu aliwataka viongozi kuhakikisha wanawaambia makocha wapya wanaokuja kuwa huku sio ulaya, hivyo wahakikishe wanawajenga wachezaji kisaikolojia ili timu ifanye vizuri.
Katika mkutano huo Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu ameweka wazi kuwa, klabu ina mpango wa kujenga ukumbi wa mikutano na ofisi katika jengo lao lililopo Mtaa wa Msimbazi.
“Awali jengo hilo ambalo ni moja ya vitega uchumi vya klabu, lilikuwa likiingiza sh. milioni 200 kwa mwaka, lakini kwa sasa linaingiza sh. milioni 500, tumezungumza mwekezaji ili klabu ijenge ofisi na ukumbi katika jengo hilo na mchakato wa ujenzi utaanza Januari mwakani,” alisema Mangungu.
Wanachama wa klabu ya Simba walitumia saa mbili katika mkutano mkuu ulioanza saa 4:02 asubuhi na kufikia tamati saa 6:00 mchana, wanachama wa klabu hiyo walijadili ajenda 10 kati ya 11 ambazo zilianishwa awali.
Ajenda ambayo haikujadiliwa ni ya kupokea na kujadili mapendekezo ya marekebisho ya kanuni za uchaguzi na katiba ya klabu.
Kati ya ajenda 10 zilizojadiliwa katika mkutano huo uliofunguliwa na Zungu aliyekuwa mgeni rasmi, ni hotuba ya mwenyekiti, kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kutoka bodi ya wakurugenzi na kupokea taarifa ya fedha zilizokaguliwa za mwaka uliopita 2020.
TAARIFA YA FEDHA
Mkuu wa Fedha, Utawala na Utendaji wa Simba, Yusuph Nassor alisoma taarifa ya fedha na kusema mwaka jana klabu iliingiza sh. bilioni 12.1 na matumizi ilikuwa sh. bilioni 12.3.
“Mo alitoa sh.bilioni 5.2 ambayo inakaribia nusu ya bajeti ambayo ni nje ya sh. bilioni 20 za uwekezaji, mwaka huu wa fedha klabu itaingiza sh. bilioni 11.8,” alisema Yusuph bila kutaja matumizi ya mwaka huu wa fedha.
Alisema katika fedha hizo, Mo ataingiza sh. bilioni 5.1 na tayari ameshatoa sh. bilioni 1.5 na sh. bilioni 1.2 zilitumika katika usajili.
Hata hivyo aliongeza klabu hiyo kama inahitaji kupambana kimataifa inapaswa kuongeza bajeti yake kwani haiwezi kushindana na klabu zenye bajeti ya zaidi ya sh. bilioni 80.
Simba itaikaribisha Red Arrows ya Zambia katika mchezo wa kwanza wa mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika, utakaochezwa Novemba 28, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya marudiano nchini Zambia Desemba 5, mwaka huu.
Na NASRA KITANA