KUNDI la vijana wadogo maarufu kama “Panya Kalowa,” limeibuka katika maeneo mbalimbli ya Jiji la Dodoma ambapo limekuwa likifanya matukio ya kihalifu na kutishia usalama wa wananchi na mali zao.
Mashuhuda wa matukio hayo, wanasema kundi hilo hujumuisha watoto wanaosoma kati ya darasa la tano hadi kidato cha kwanza ambao hutembea nyakati za usiku kwa makundi ya watu kati ya 12 hadi 19.
Akizungumzia hali hiyo, Mkazi wa Medeli, Dotto Kusulya, alisema wengi wa vijana hao ni wanafunzi wa sekondari ambao wamekuwa wakijificha katika vichaka kuvizia watu wanaopita kisha kuwapora.
“Jirani na nyumba yangu kuna vichaka, wanafunzi hawaendi shuleni hutumia vichaka hivyo kujificha na kuwatendea vitendo vya ajabu watoto wadogo. Juzi, walimpora mfanyabiashara wa mayai aliyekuwa akipita eneo hilo.
“Walimuita kijana huyo kwa lengo la kutaka kununua mayai lakini kwa sababu walikuwa wengi, walimpora mayai yote na kumpiga. Niwaombe wazazi wafuatilie mienendo ya watoto wao wajue kama wanafika shuleni au la,” alieleza.
WACHIMBA HANDAKI
Katika hali isiyokuwa ya kawaida vijana hao wamechimba shimo ambalo wanalitumia kujificha pindi wanapofanya matukio ya kihalifu.
Mkazi wa Dodoma Makulu, Samson Mkopi, alisema hivi karibuni waliwakamata vijana watatu katika eneo la Kanisa la Mzee Mongi.
Alisema vijana hao, walikutwa wamechimba handaki katika maeneo hayo ambapo juu, waliweka nyasi na kulitumia eneo hilo kama maficho yakihusisha wanafunzi wa shule za misingi na sekondari.
“Kuna matendo ambayo wao wanayafanya kama uvutaji bangi na kushiriki ngono. Siku hiyo walipokimbizwa katika eneo hilo, ndani ya shimo walitoka watoto zaidi ya 19.
“Baada ya kukimbia, walisahau simu na redio kadhaa ndogo, lakini muda si mrefu alifika kiongozi wao ambae ameunda kikundi hicho kwa ajili ya kuwafundisha ngumi na kuvuta bangi akidai amefuata vitu vya vijana wake,” alieleza.
Alisema polisi jamii walifika katika eneo hilo na kufanikiwa kumkamata kijana huyo ambaye alipelekwa kituo cha polisi.
WACHIMBA HANDAKI
Katika hali isiyokuwa ya kawaida vijana hao wamechimba shimo ambalo wanalitumia kujificha pindi wanapofanya matukio ya kihalifu.
Mkazi wa Dodoma Makulu, Samson Mkopi, alisema hivi karibuni waliwakamata vijana watatu katika eneo la Kanisa la Mzee Mongi.
Alisema vijana hao, walikutwa wamechimba handaki katika maeneo hayo ambapo juu, waliweka nyasi na kulitumia eneo hilo kama maficho yakihusisha wanafunzi wa shule za misingi na sekondari.
“Kuna matendo ambayo wao wanayafanya kama uvutaji bangi na kushiriki ngono. Siku hiyo walipokimbizwa katika eneo hilo, ndani ya shimo walitoka watoto zaidi ya 19.
“Baada ya kukimbia, walisahau simu na redio kadhaa ndogo, lakini muda si mrefu alifika kiongozi wao ambae ameunda kikundi hicho kwa ajili ya kuwafundisha ngumi na kuvuta bangi akidai amefuata vitu vya vijana wake,” alieleza.
Alisema polisi jamii walifika katika eneo hilo na kufanikiwa kumkamata kijana huyo ambaye alipelekwa kituo cha polisi.
WENYEVITI WAELEZA
Mwenyekiti wa Mtaa wa Njedengwa, Daimu Haji, alisema vijana wanaojiita Panya Kalowa, asilimia kubwa wanatoka katika mtaa wake.
Alisema vijana hao wengi wanasoma shule za msingi kuanzia darasa la tano ikizidi sana kidato cha kwanza.
Haji alisema vijana hao mara nyingi wanashinda katika eneo ambalo reli ya kisasa inajengwa na wanapoona polisi katika maeneo hayo hukimbia kushuka mitaa ya Njedengwa.
“Wiki iliyopita tulipata taarifa kuwa vijana wanaosoma Shule ya Msingi Medeli kati ya darasa la tano na sita, wametekwa. Tukio hilo lilifanywa na vijana wawili mmoja wa kidato cha kwanza mwingine darasa la sita ambao waliwapeleka korongoni wakawapa adhabu na
kuwanyang’anya fedha walizokuwa nazo. “Baada ya kuwatambua vijana hao na kuletwa kwetu, tuliita askari wakawapeleka kituoni lakini waliachiwa kwa sababu walitakiwa
kupewa adhabu kwani ni vijana wadogo sana. “Hivi ninavyoongea hata kukitokea sherehe ndogo ikifika saa moja usiku kundi la Panya Kalowa wanakuja na mapanga, utachagua kufunga mziki au watu kuuana kimsingi
tunashindwa kwa sababu ni vijana wadogo.”
WASHUSHA KIPIGO MSIBANI
Diwani wa Kata ya Dodoma Makulu, Fadhili Chibago, alisema hali ya usalama katika kata hiyo siyo nzuri kutokana na changamoto ya matukio ya kihalifu.
“Kuna tukio limejitokeza wakati watu wameenda msibani kiliingia kikundi cha vijana 19 kati ya umri wa miaka 12 hadi 18, wakapiga watu na kuchukua vitu vingi. Kuna dada alikuwa anafanya kazi jiji alivamiwa na vijana wanosadikika ni Panya Kalowa kisha kupigwa vibaya na baada ya siku tatu alifariki,” alisema.
CCM YAELEZA
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma,Pili Mbanga, alisema Chama hakitahusika na mzazi ambaye mtoto wake atatiwa hatiani kwa kosa la kufanya uhalifu.
Pili aliwaelekeza wenyeviti wa mitaa na mashina kuhakikisha wanaweka ulinzi shirikishi na kurudusha utaratibu wa zamani wa kufuatilia wakazi wa maeneo yao.
KAULI YA MKURUGENZI
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru, alisema kutokana na malalamiko ya wananchi kuhusu kuwepo kwa viwanja vingi ambavyo havijaendelezwa kwa muda mrefu hivyo kutengeneza vichaka kuwa maeneo ya kujificha kwa waalifu, wataanza kuchukua hatua.
Alisema wataanza kuchukua hatua ya kunyang’anya viwanja hivyo kwa kufuata Sheria ya Ardhi ambayo inasema mmiliki wa kiwanja asipoendeleza ndani ya miezi 36, kiwanja hicho huchukuliwa na kugawiwa kwa mtu mwingine.
MKUU WA WILAYA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, ametoa wiki mbili katika mitaa yote ya Kata ya Dodoma Makulu kuanzisha polisi jamii.
Alisema wilaya ipo tayari kutoa ushirikiano wa vifaa, mafuta na mambo mengine ili polisi jamii wapate mafunzo kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya kihalifu.
RPC DODOMA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Otieno Martin, alisema ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananchi kwa sababu, idadi ya polisi ni ndogo ukilinganisha na maeneo yaliyopo.
Aliwataka wananchi kuanzisha ulinzi shirikishi ili mitaa iwe salama kwa sababu mhalifu anapofanya vitendo vya kihalifu haangalii.
KAULI YA MBUNGE
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, aliwataka wakazi wa maeneo ya Kisasa kufunga kamera katika maeneo yao ili kukomesha vitendo vya kihalifu.
Mavunde alisema pia kutokana na uhalifu unaoendelea kushamili katika maeneo hayo ni vyema madereva bodaboda wanaofanyakazi usiku kupewa utambulisho maalumu na namba kuwabaini wahusika wa vitendo hivyo.
MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka, alisema kila mzazi anapaswa kumkanya mtoto wake na kila kijana anapaswa kuchunga miendendo yake ili baadaye lawama zisitokee.
Aliwataka wazazi ambao wana watoto ambao ni vibaka wachukue hatua mapema kwani askari watafanya kazi yao.
Na FRED ALFRED, Dodoma