MATUKIO mawili yametokea kwa nyakati tofauti mkoani Dar es Salaam na kuibua hisia kwa wakazi wake, hali iliyolisukuma Jeshi la Polisi kuapa kupambana usiku na mchana kuhakikisha linawanasa wote waliohusika.
Tukio la kwanza linahusu kuokotwa maiti za watoto wachanga mapacha, zilizotelekezwa katika dampo la Mbezi Luis, Manispaa ya Ubungo, huku la pili likihusisha mauaji ya mwanamke baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani na tumboni na mtu aliyedaiwa mume wake, wilayani Ilala.
KAULI ZA POLISI
Akithibitisha kutokea kwa tukio la kwanza, Kamanda wa Polisi Kinondoni, Ramadhan Kingai, amesema tukio hilo lilitokea Juni 6, 2022, ambapo uchunguzi wa awali umebaini maiti za watoto hao zilitelekezwa baada ya mwanamke kujifungua na kisha kuwaacha eneo hilo.
“Ni kweli tukio hilo limetokea, mwanamke alijifungua watoto mapacha lakini walikutwa wakiwa wamefariki duniani. Bado tunaendelea kufuatilia ni nani amefanya kitendo hicho,” alisema.
Miili ya watoto hao ilionekana juzi katika dampo lililopo karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli.
MASHUHUDA
UHURU ilizungumza na baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, wakiwemo wafanyabiashara na wafanya usafi wa kituo hicho cha Magufuli, ambao walisema walishuhudia maiti za watoto hao, saa 12:00 asubuhi.
Mariam Said, mfanyabishara wa duka la nguo, jirani na kituo hicho cha mabasi; alisema alishuhudia maiti za watoto wachanga waliolazwa chini ya takataka na kufunikwa na kanga.
POLISI TENA
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amezungumzia tukio la pili la mauaji ya mwanamke na kusema, polisi wanaendelea kumtafuta mtu aliyehusika na mauaji hayo.
Alisema mwanamke huyo aliyetambuliwa kwa jina la Logesara Chitemo, mfanyabiashara wa pombe za kienyeji na mkazi wa Ukonga Mazizini, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam, aliuawa Juni 6, mwaka huu, saa 3:00 usiku.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linaendelea kumtafuta mtu mmoja anayetuhumiwa kumuua mke wake, aliyefahamika kwa jina la Logesara Chitemo, huyu ni mgogo aliyekuwa anafanya biashara ya pombe ya kienyeji.
“Mtu huyo alifariki dunia baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya tumboni na kifuani tarehe sita, mwezi wa sita, mwaka 2022 majira ya saa tatu usiku, upelelezi unaendelea na jeshi limeapa lazima mtuhumiwa huyo atakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema
Mauaji ya mwanamke huyo Dar es Salaam, yametokea ikiwa imepita wiki moja tangu kutokea kwa mauaji mengine mkoani Mwanza, ambapo mwanaume mfanyabiashara alimuua mke wake kwa kumpiga risasi, kwa kile kinachodhaniwa ni wivu wa mapenzi.
IRENE MWASOMOLA Na JULIETH MLWATI (DSJ)