WAZIRI wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo (Mb), ametoa ufafanuzi wa taarifa ya mapendekezo ya ukarabati wa Jengo la Madini katika Maonesho ya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba) na kuitwa jina la Hayati Dk. John Magufuli, ambapo pia imependekezwa kujegwa sanamu ya Hayati Magufuli.
Akizungumza katika mahojiani maalumu na kituo cha redio cha Efm cha Dar es Salaam, Profesa Mkumbo ameyasema, Benki ya NBC ndio wadhamini wakubwa wa maonesho ya 45 ya sabasaba,yaliyofikiwa tamati leo.
Waziri huyo amesema moja ya makubaliano ya udhamini huo, ni kufanya ukarabati wa mabanda mawili kwa gharama ya sh.milioni 420, ambazo ni fedha za Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) sio za Serikali wala za mkopo, lakini ni sehemu ya udhamini wao.
Aidha, Mabanda yanayokarabatiwa kwa udhamini huo, hutajwa majina ya Marais wastaafu, na kwamba moja ya banda ambalo ni la Madini, limependekezwa kutajwa jina la Magufuli, ambapo tayari wameomba kibali kwenye Mamlaka ili kutaja jina hilo.
Profesa Mkumbo ameendelea kueleza kuwa: “Moja ya mapendekezo ya Benki ya NBC, wakikarabati banda waruhusiwe kujenga na sanamu ya Hayati Magufuli, ni mapendekezo yao ambayo yamewasilishwa serikalini, yanasubriwa kufanyiwa kazi na hayajapata majibu kwa hiyo nisisitize hakuna uamuzi uliofanyika, lakini muhimu zaidi fedha zinazozungumuzwa, sh. milioni 420 sio fedha za serikali ni fedha za NBC kama sehemu ya ufadhili wao.”
Na Pius Ntiga



























