MKUU wa Wilaya Temeke, Jokate Mwegelo, ameipongeza Kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa ushirikiano wanoutoa kwa serikali wa kutoa ajira kwa vijana kupitia vituo vyao vya mafuta vinavyopatikana kote nchini.
Jokate alitoa pongezi hizo wakati akizindua Wiki ya Huduma kwa Wateja na kuzindua kituo kipya cha mafuta kilichopo Sokota, Temeke jijini Da r es Salaam.
”Puma wanaongoza kwa huduma nzuri na bidhaa bora za mafuta na vilainishi ambavyo vina viwango vya kimataifa vyenye kukidhi mazingira na watumiaji wake, Katika kukabiliana na soko la ajira Puma Energy wamekuwa wakishirikiana na Serikali kwa ukaribu zaidi kwa kutoa ajira kwa kundi kubwa la vijana na ajira hizo zina miiko na maslahi kwa wafanyakazi wake.” Amesema Jokate
Alisema kampuni hiyo imekuwa ikishiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi jambo linaloungwa mkono na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mamlaka za TARURA, na TANROAD kwa kuwaelimisha wanafunzi na jamii kwa ujumla kupitia kampeni mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinapunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo na ulemavu.
Jokate ameeleza ongezeko la vituo vya Puma hasa katika maeneo ambayo hayakufikiwa na huduma hiyo kunakwenda sambamba na azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan yenye mlengo katika uwekezaji na kuzalisha ajira kwa watanzania.
Kuhusiana na wiki ya huduma ya wateja, Jokate amesema kampuni hiyo imekuwa ikijali watanzania kupitia bidhaa zao za mafuta, vilainishi na maduka yanayopatikana katika vituo vyao na kupitia wiki hiyo ya wateja watapata matokeo chanya ya kuboresha huduma zao baada ya kusikiliza maoni na mapendekezo kutoka kwa wateja wao.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Meneja Uendeshaji wa Huduma kutoka Puma Energy Lameck Hiliyahi amesema, kampuni hiyo ina ubia na Serikali kwa asilimia 50 kwa 50 na kipaumbele chao ni kutoa huduma bora kwa wateja kupitia bidhaa za mafuta, vilainishi na maduka yanayopatikana katika vituo vyao vya mafuta.
Alisema maadhimisho hayo yaliyobebwa na kauli mbiu ya ‘Huduma Nzuri kwa Wateja’ wateja watapata fursa ya kutoa maoni yao, mapendekezo, ushauri pamoja na kujishindia zawadi mbalimbali na kueleza kuwa tangu kuanzishwa kwa wiki hiyo ya wateja 2019 wamekuwa wakipata manufaa kupitia wateja wao.
”Tumekuwa tukishirikiana na Serikali kwa ukaribu zaidi katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana, tumeajiri vijana wengi katika vituo vyetu vya mafuta, walinzi na wafanyakazi katika maduka yote ya Puma Energy na hii ni kwa vituo vyote nchini.” Amesema.
Naye Meneja wa Mauzo ya rejareja wa kampuni hiyo, Venessy Chilambo, amesema wiki ya huduma kwa wateja ni fursa kwao kwa kuchukua mrejesho kutoka kwa wateja na kuifanyia kazi ili kuboresha huduma na maadhimisho hayo yanaadhimishwa katika vituo vyao.
Venessy ameshauri wateja na watanzania kwa ujuma kutumia bidhaa na kufurahia huduma zinazotolewa na kampuni hiyo kwa usalama wao binafsi na vyombo vya moto.