CHAMA Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Utafiti, Sayansi, Habari na Ufundi Stadi (RAAWU), imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa usikivu wake na kupandisha mishahara kwa asilimia 23.3 huku wakimuomba kuingilia kati sekta binafasi ambayo imeachwa pasipo kuguswa tangu mwaka 2013.
RAAWU imesema, waraka wa mwisho wa mishahara katika sekta binafsi ulitolewa mwaka 2013 na kwa kuwa bodi ya kima cha chini cha mishahara katika sekta binafsi imekwishaundwa, kuna haja ya serikali kuingilia kati ili bodi hiyo itangaze mishahara.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa RAAWU Taifa, Jane Mihanji, amesema hatua ya Rais Samia Samia kuongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa kiwango cha asilimia 23.3 ni ya kupongezwa.
Amesema, hatua hiyo itachochea maendeleo nchini kuleta ari ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma na kuongeza tija ya ufanisi.
Amebainisha kuwa pamoja na kupandisha mishahara hiyo katika sekta ya umma, RAAWU inamuomba Rais Samia, kuingilia kati sekta binafsi ambayo imeachwa pasipo kuguswa tangu mwaka 2013 ambapo ndipo waraka wa mwisho ulipotolewa.
“Kwa kuwa bodi ya kima cha chini cha mishahara katika sekta binafsi imeundwa bodi hii pia itangaze mishahara ya sekta binafsi,”amesema.
Jane ameongeza kuwa, RAAWU inawasihi wafanyakazi katika sekta ya umma na sekta binasfi kuongeza bidii katika utendaji kazi ili kuijengea uwezo serikali kutokana na tija ya utendaji huo.
Ameeleza kuwa, ili kumdhihirishia Rais Samia kuwa nyongeza ya mishahara aliyoitoa kwa watumishi wa umma imekuwa na faida kwa serikali unahitajika utendaji wenye tija.
“Hatua ya kuruhusu upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wa umma ambao ulisimama muda mrefu ni ya kupongezwa kwa kuwa Rais Samia amewapandisha madaraja watumishi 190,781 na kiasi cha sh. 39,649,999988,204 zilitumika kuwalipa watumishi katika upandaji huo wa madaraja hayo,”amesema.
Aidha, Jane amesisitiza kuwa, Rais Samia amelipa malimbikizi ya mishahara na madai ya watumishi wa umma sh.bilioni 91.9 na kuruhusu wafanyakazi 19,386 kubadilishiwa kada na kulipwa zaidi ya sh.bilioni 1.3.
Amesema kilio cha mishahara kwa watumishi ni cha muda mrefu ambapo RAAWU, walimuomba Rais Samia kuongeza mshahara kwa kima cha chini cha sh. Milioni 1.1 na Rais alieleza kuwa mishahara itapanda lakini si kwa kiwango hicho na badala yake itapanda kulingana na kukua kwa uchumi.
“Kilichopitishwa RAAWU tumeridhia, kwakuwa nchi ilipitia katika majanga mengi ikiwemo UVUKO-19, lakini Rais wetu ni msikivu ameona haja ya kupandishi mishahara tunachoweza sema tuna deni kwa Rais Samia katika kuhamasisha utendaji bora kwa wafanyakazi,”amesema.
Na Mariam Mziwanda



























