MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amempongeza Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuwa kiongozi wa mfano visiwani humo.
Kauli hiyo aliitoa katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani iliofanyika jana kwenye ukumbi wa Sheikh Idris Abdul-Wakil mkoa wa Mjini Magharibi.
Makamu huyo wa Rais aliwashauri viongozi wengine kufuata mfano wake kwa kuweka wazi mambo yanayohitaji kuwekwa na serikali.
“Tunafahamu jinsi ambavyo baadhi ya viongozi wa serikali, taasisi za umma na jumuiya za kiraia wanavyoficha habari hasa zile zinazotoa sura mbaya au kukosoa vitendo vyao, wote hawa
hupendelea wasifiwe tu na kupongezwa,”alisema Othman.
Alisema baadhi ya viongozi kuwafukuza waandishi kwa kuwakaripia na hata kuwatisha wanapotafuta undani wa suala lenye harufu ya uzembe, ubadhirifu, rushwa na ufisadi.
“Kwa namna ya kipekee katika hili tumpongeze Rais Dk. Mwinyi kwa kutuonyesha njia katika mkutano yake ya kila mwezi na waandishi wa habari na uhuru aliutoa katika kuhojiwa masuala mbalimbali
kwa kweli ni mfano wa kuigwa,”alisema.
Kwa upande wake mwandishi wa habari, Tabia Makame alisema kuna sababu ya waandishi kujiongeza elimu na maarifa ili kuwa na ufanisi mzuri wa kazi.
HANIFA RAMADHANI, ZANZIBAR





























