RAIS Samia Suluhu Hassan, amehitimisha kilio cha muda mrefu cha utekelezaji mradi wa maji katika miji 28 nchini ambapo ameshuhudia utiaji saini wa mradi huo utakaogharimu zaidi ya sh. trilioni moja.
Mradi wa maji katika miji 28 ni wa kwanza kwa ukubwa katika historia ya nchi kutekelezwa kwa pamoja ambao unatarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya milioni sita huku fedha zingine zikipelekwa kutatua changamoto ya maji upande wa Zanzibar.
Mji itakayonufaika kupitia mradi huo ambao fedha zake ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Exim ya nchini India, ni Handeni, Muheza, Pangani, Kilwa masoko, Newala, Ifakala, Chunya, Songea, Njombe, Lujewa, Makambako, Wanging’ombe, Mafinga, Nanyumbu, Mpanda, Sikonge, Urambo, Kaliua, Singida, Manyoni, Chemba, Chamwino, Kasulu, Kayanga, Geita, Rorya, Tarime na Chato.
Akizungumza Ikulu Chamwino nje kidogo ya Jiji la Dodoma wakati wa halfa ya utiliaji saini baina ya serikali na wakandarasi wataotekeleza mradi huo kwenye maeneo husika, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema serikali inaendelea kudumisha huduma muhimu kwa wananchi.
Alisema shughuli hiyo inafanyika kwa kutumia fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali na fedha za wadau wa maendeleo.
“Mradi huu ni matokeo ya ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na Serikali ya India ambapo India imetoa mkopo wa dola milioni 500 kuwezesha mradi huo mkubwa zaidi kutekelezwa kwa pamoja ndani ya nchi.
“Serikali ya India imekuwa mshirika mkubwa kupitia Benki ya Exim ya India ambayo iliwezesha utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria wenye thamani ya sh. bilioni 617 ambao umepelea maji Tabora, Igunga na Nzega. Kupitia mradi huo vijiji 102 na kazi ya usambazaji maji inaendelea hadi Shinyanga,”alisema.
Alimpongeza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kwa kufanikisha mradi huo wa miji 28 huku akisisitiza hakuna mji utakaoachwa.
“Wizara ya Maji mmebadilika sana. Mlinipa tabu mwanzo tulielezana kweli na sasa tunakwenda vizuri. Mradi huu badala miji 16 tumekwenda miji 28, hata miradi tunayotekeleza sasa mmejitahidi kubana matumizi, mradi mmoja unazaa fedha kuendeleza mradi mwingine.
“Tumefanya kazi nzuri kuokoa mradi wa visima 10 kila mkoa, tumekuta kuna visima maji hayatoki, kuna miundombinu chanzo hakuna, nikamwambia Aweso sitaki upuuzi nendeni mkaangalie wapi kuna tatizo na sasa mmetatua, Huo ndio uzalendo tunaoutaka,” alisisitiza.
Rais Samia aliiagiza wizara hiyo kusimamia mradi hadi maji yapatikane kwa kuhakikisha wakandarasi wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Huu ni mkopo na zote zinakwenda katika maji, kwa sababu ni mkopo Watanzania wote tutakuja kulipa, nendeni mkasimamie mradi ulete manufaa,” alieleza.
Alisema serikali itaendelea kujenga miradi ya maji kila eneo la nchi ikiwa ni utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoelekeza ifikapo mwaka 2025, huduma ya maji safi na salama inafikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.
“Kuna dalili zote kwamba tunaweza kwa sababu mpaka hapa tulipo kwa vijijini tumefikia asilimia 74 lakini miradi 1,000 inayoendelea vijijini Tanzania nzima inakwenda kuchangia asilimia nne, kwa hiyo mpaka Juni mwakani tutafikia asilimia 78 na tuna miaka mingine miwili ya utekelezaji miradi ya maji itakayotufikisha asilimia 85.
Kwa upande wa mjini alisema: “Tupo asilimia 86.6 nipongeze Dar es Salaam karibu wanafikia asilimia 100, wapo asilimia 96. Miradi hii itakayosainiwa itatufikisha asilimia nane na itakwenda kwenye miji, tupo asilimia 86 kwa hiyo tukijumlisha tutafikia asilimia 94.5. Hivyo tunaweza kufika au kupita kama tulivyoelekezwa na ilani.”
Kuhusu mradi wa maji kwa miji ya Same na Mwanga alisema serikali imeshatatua changamoto ya kisheria na inaendelea kutafuta fedha ili ifikapo mwakani mradi huo uanze kutekelezwa.
“Tutakwenda kutafuta fedha kuhakikisha mradi huo wakati wenzao wa miji 28 wakipata maji na wao waate maji,” alisisitiza.
Aisema kwa Dodoma serikali ina mpango wa kujengwa bwawa la maji Farkwa lakini pia kutoa maji Mtera kupeleka maji Jiji la Dodoma angalau kwa asilimia moja.

WAZIRI WA MAJI
“Ulitueleza wakinamama wanatembea umbali mrefu kufuata maji, maelekezo uliyotupa hutaki kusikia wala kuona wakinamama wanateseka kwa changamoto ya maji. Ulituelekeza ipo miradi ambayo maji yanatoka wakati wa uzinduzi pekee na miradi kutekelezwa kwa fedha nyingi bila halisia.
“Baada ya maelekezo nilikaa na wataalamu, watendaji wetu kwa sasa wana moyo wa kazi, tulikuwa wakali sana kuona mkandarasi pindi anapofanya vibaya. Mradi huu baada ya kutupa maelekezo tuliota maelekezo ulipaswa kutelelezwa miji 16 Bara na mmoja Zanzibar lakini tunakwenda kutekeleza miji 28,” alieleza.Alisisitiza kuwa wizara yake
watausimamia, kuufuatilia usiku na mchana kuhakikisha maelekezo ya kumtua mwanamke kichwani yanatimia.
“Mwaka wako mmoja bajeti tumetekeleza kwa asilimia 95, mwaka huu tulivyoisoma bajeti imepitishwa kwa asilimia 100 haijawahi kutokea. Hakuna mbunge aliyesema hapana. Hii ni imani kubwa kwa wabunge, Wizara ya Maji miaka ya nyuma uitekelezaji wake ulikuwa sio wa kuridhisha,” alisema.
Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Pangani (CCM) alisema wizara hiyo ilikuwa na miradi chechefu 177 ambapo hadi sasa miradi 126 imekwamuliwa.
Pia, alisema katika mwaka ujao wa fedha serikali kupitia Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) inakwenda kutekeleza miradi ya maji 1,029, ujenzi wa miradi 232 kila jimbo kupitia fedha za Uviko-19, ununuzi wa mitambo ya kuchimba visima kila mkoa na ununuzi wa seti ya mitambo mitano ya kuchimba mabwawa itayopokelewa mwezi huu.
Katika kuhakikisha wananchi wanauziwa maji kwa bei stahiki, Awezo alisema mwezi huu wizata itatoa bei elekezi ya maji kuwawezesha wananchi kunufaika na huduma hiyo.
CCM YAKOSHWA NA KASI YA RAIS SAMIA
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Christine Mndeme, alisema CCM inampongeza Rais Samia kwa kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama kwa vitendo ambapo Dunia inashudia.
“Pongezi hizi zimekuwa zikitolewa na makundi mbalimbali ndani ya Chama na serikali kwa kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo. Leo historia inakwenda kuandikwa Tanzania kwani zaidi ya sh. trilioni moja sio kazi ndigo.
Aliongeza kuwa: “Mwanamke wa Kitanzania badala ya kutumia muda mrefu kufuata maji, atatumia muda mwingi katika shughuli za maendeleo. Sekta ya maji ni muhimu kwa sababu maji hayana mbadala. Tunakupongeza Rais wetu kwa moyo wa upendo kwa Watanzania.”
Alisisitiza kuwa wakandarasi watakaopewa kazi ya kutekeleza miradi hiyo waitekeleza kwa umakini, ndani ya bajeti na viwango vinavyohitajika.

KAULI YA BUNGE
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema Bunge linampongeza Rais Samia kwa sababu hatua anazozichukua zinawasaidia wananchi.
“Katika ujenzi wa barabara, wananchi anapata fursa kusafirisha mazao, kusafiri, mikoa na wilaya zinaunga na tunaamini hata vijiji na vitongoji vitaungana.
“Bajeti ya maji ilipitishwa kama ilivyokuwa inaombwa na serikali pamoja na fedha hizi ambazo tuliahidiwa zinatafutwa lakini hapa tunashuhudia hazitafutwi, zimepatika. Tumeshuhudia namna ambavyo asilimia nane za upatikanaji maji zinaongezeka kupitia mradi huu wa miji 28,” alieleza.
Spika alisema wabunge walikuwa wakiusuburi mradi huo tangu mwaka 2015 ambapo huduma hiyo ya maji itakwenda kuwanufaisha wananchi ambao waliahidiwa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
“Tunafahamu nia yako sio kufikia asilimia 95 mijini na 85 vijijini, tunafahamu dhamira yako ni kufikisha maji asilimia 100 mijini na vijijini,” Dk. Tulia alibainisha.
TAMISEMI YASISITIZA USIMAMIZI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa, alieleza kuwa tangu mwaka 2015 alipoingia bungeni mradi huo ulikuwa ukizungumzwa lakini sasa unatekelezwa.
“Kila siku Rais Samia amekuwa akileta mageuzi katika kutekeleza dhamira ya kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani. Trilioni 1.73 ni fedha nyingi, TAMISEMI katika bajeti tumepanga kukusanya sh. trilioni 1.01 ukichukua makusanyo yote ya halmashauri kwa mwaka mzima, lakini fedha hizo zinakwenda kutekeleza miradi ya maji.
WAZIRI MKUCHIKA
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, alisema awali wimbo wa mkopo wa Exim Bank kutekeleza mradi huo walilazimika kuwaambia wananchi wasiwe na wasiwasi kwamba serikali imepata mikopo, lakini kilichotokea ni hali mbaya ya maji.
“Kama Mbunge ninayetokea kwenye mradi wa maji wa Makonde, mwaka jana tulinunua dumu la maji kwa sh. 2000. Kule Mtwara tumekubaliana baada ya shuhghuli hii, waziri atakuja kutukabidhi mkandarasi ngoma zitachjezwa hadi asubuhi. Tunakushukuru Rais Samia kusaidia kupatikana mkopo huu. Nikushukuru kwa jitihada za kutunusuru walengwa ambao tutanufaika na mradi huu,” alieleza
INDIA KUENDELEZA USHIRIKIANO
Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Slikanta, alisema tukio hilo ni ushahidi kwamba serikali ya India itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali hususan ya maji.
Alisema kusainiwa kwa mkataba huo una ongezeza thamani ya miradi ya maji inayofadhiliwa na India kufikia dola bilioni moja ambapo alisisitiza wakandarasi kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia ubora na kwa wakati.
Alieleza kuwa atasimamia mradi huo kuhakikisha unatekelezwa kwa viwango ambapo India itaendelea kuongeza ushirikiano na Tanzania kwani zipo kampuni nyingi za India zinahitaji kuwekeza kwenye sekta ya bandari, madini na biashara.
Balozi huyo alieleza kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia India na Tanzania zitaendelea kushirikiana zaidi kwani Tanzania ndio mshirika mkubwa wa India katika miradi ya maji.
Alisema serikali ya India imeondoa ushuru kwa bidhaa za Tanzania zinazosafirishwa kwenda India ambapo mauzo yameongezeka kufikia dola bilioni nne.
WATU MILIONI SITA KUNUFAIKA
Akitoa taarifa fupi kuhusu mradi huo wa miji 28, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Antony Sanga, alisema mradi huo wenye thamani ya dola milioni 500 unatekelezwa kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya Exim ya India.
Alisema dola milioni 465 zitatumika Tanzania Bara huku dola milioni 35 zimepangwa kutumika Zanzibar.
“Mradi huu ni wa kihistoria kwa nchi kwa sababu ni mkubwa kuliko yote iliyowahi kutekelezwa. Wakandarasi jambo la msingi wakazingatie ubora wa ujenzi wa mradi, muda na wazingatie gharama. hatutarajii kuona wanaanza kuongeza gharama.
“Ilizoeleka kipindi cha nyuma badala ya kuajili wataaluamu wa kutekeleza mradi, wanaajiri wwataalamu kuangalia wapi wakadai pesa zaidi,” alieleza.
Mhandisi Sanga alisisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha watu milioni sita ikiwa ni ongezeko la asilimia nane la wanufaika wa maji maeneo ya mijini.
Na MUSSA YUSUPH, Dodoma