Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi kama ifuatavyo:
Amemteua Dkt. Mursali Ally Milanzi kuwa Naibu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya Mipango ya Kitaifa. Kabla ya uteuzi huu, Dkt. Milanzi alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango ya Kitaifa katika Tume ya Mipango.
Aidha, Dk. Samia amemteua Dkt. Lorah Basolile Madete kuwa Naibu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya Ubunifu wa Biashara. Kabla ya uteuzi huu Dkt. Madete alikuwa Meneja wa Idara ya Uchumi Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Mwanza.
Vilevile, memteua Dkt. Linda Ezekiel kuwa Naibu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya Menejimenti ya Utendaji na Tathmini. Dkt. Ezekiel alikuwa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, President’s Delivery Bureau (PDB).
Pia amemteua Bw. Alban Mark Kihulla kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA). Kabla ya uteuzi huu Bw. Kihulla alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Amemteua Prof. Najat Kassim Mohamed kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC). Kabla ya uteuzi huu Prof. Najat alikuwa Naibu Mkuu wa Chuo (Mipango, Utawala na Fedha), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Aidha, amemteua Bi. Bernadetta Nagonyani Ndunguru kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET). Bi. Bernadetta ni Mkurugenzi wa Mafunzo Mstaafu, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).