RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Nchini, IGP Simon Sirro, kuangalia sababu za idadi kubwa ya askari wanaohitimu mafunzo kupenda kupangiwa kitengo cha usalama barabarani.
Pia Rais Samia alimtaka IGP Sirro kumpelekea majibu kinachosababisha idadi kubwa ya askari kuomba kupangwa kikosi cha ‘traffic’ na bandarini.
Agizo hilo alilitoa Novemba 23, 2021, wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani jijini Arusha, iliyobeba kaulimbiu isemayo ‘Jali Maisha Yako na Wengine Barabarani’.
Alisema idadi kubwa ya askari wanapomaliza mafunzo, hutafuta nafasi ili wapangwe katika kikosi cha usalama barabarani na sio sehemu nyingine, jambo ambalo linatia shaka.
“Askari wengi wanapomaliza mafunzo yao kuna ‘lobbing’ kubwa na maombi ya kupangwa kwenye kikosi cha ‘traffic’, unajiuliza kwani kuna nini huko, mbona hawaendi kuomba kupangwa kwenye malindo ya viongozi,” alihoji.
“Nilishawahi kuona vijana kijijini kwetu wamemaliza mafunzo, wakaja kuniomba, niwaombee wapangiwe traffic, nikamuuliza wa kwanza kwanini unaomba upangwe traffic.
“…akasema unajua ukienda traffic maisha yanakwenda haraka unanyanyuka haraka, lakini wa pili alinijibu kule kwetu kuna askari anaitwa cheupe anaongoza misafara ya viongozi, ana mbwembwe kweli kweli akiwa njiani kwa hiyo aliniambia anamuhusudu sana cheupe anataka apewe pikipiki afanye kama yeye,” alisema.
Kuhusu ajali za barabarani, Rais Samia alisema asilimia 90 ya makosa yanatajwa kutokana na sababu za kibinadamu, hivyo hapana budi kujirekebisha.
Alitaja ajali zinazosababishwa na madereva wa magari binafsi ni 535, malori 209, mabasi ya abiria 148 na daladala ni 142, hiyo ni kwa kipindi cha miaka mitano.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Hamis Hamza Chillo, alisema majukumu yao ni kuratibu, kuelimisha na kushauri namna ya kutafuta suluhisho ya ajali za barabarani.
Alisema baraza hilo limeandaa mpango mkakati wa kupunguza ajali hizo, ikiwa ni muendelezo wa juhudi za kukomesha matukio hayo.
Hata hivyo, aliomba baraza hilo kuangaliwa kwa jicho la pekee ili kuliwezesha kifedha kutekeleza majukumu ambapo kwa sasa linategemea michango ya wadau.
Aidha, IGP Sirro, alisema hali ya usalama ni shwari nchini na jeshi la polisi litaendelea kudhibiti wachache wanaohatarisha amani kwa maslahi binafsi.
Alisema kati ya Janauri hadi Septemba mwaka huu, makosa ya jinai ni asilimia 3.9 na makosa ya usalama barabarani ni asilimia 15.4.
Akitoa taarifa ya hali ya usalama barabarani nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Willbroad Mtafungwa alisema hali imeimarika na ajali zimepungua.
Alisema hatua hiyo imetokana na utoaji wa elimu, usimamizi wa sheria na ufanyaji wa operesheni mbalimbali kwa watumiaji wa barabara.
Alibainisha katika utoaji elimu wameshatangaza vipindi vya redio 2,284 sawa na ongezeko la asilimia 46 kutoka mwaka jana 1,627, televisheni 136 sawa na asilimia 47.8 kutoka vipindi 92 mwaka jana.
Alisema kwa mwaka huu kuanzia Januari hadi Septemba elimu imetolewa kwa shule za msingi 3,825 na wanafunzi 657,934.
Alitaja idadi ya abiria waliopewa elimu ni 9,883,673, madereva 551,968 wa sekta binafsi na umma 6,827.
Alieleza kwa kipindi hicho madereva 537 wamefungiwa leseni zao za udereva baada ya kuonekana sugu huku 472 wakifikishwa mahakamani na wengine wameadhibiwa.
Alisema takwimu za ajali kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2018 matukio yalikuwa 3,732 vifo 1,788 na majeruhi 3746.
SACP Mtafungwa alisema mwaka 2019 matukio ya ajali yalikuwa 2,704, vifo 1440 na yamepunguza kwa asilimia 19.5 na majeruhi 2,830.
Aliongeza mwaka 2020 matukio yalikuwa 1,714 vifo 1,270 na majeruhi 2,126.
“Katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu, ajali zilikuwa 1,187, vifo 900 na majeruhi ni 1,405,” alisema.
Maximillian Mapunda ni Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), alisema wamepewa jukumu la kufuatilia utekelezaji wa mpango wa dunia wa miaka 10 wa kupunguza ajali na majeruhi barabarani.
Alisema mpango huo ulizinduliwa Oktoba mwaka huu, ukihusisha ushirikiano wa UN na wadau mbalimbali wenye lengo la kupunguza asilimia 50 ya vifo na majeruhi wa ajali za barabarani.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, alisema wanaheshimu mchango unaofanywa na Rais Samia katika kuimarisha usalama barabarani.
Na JUMA ISSIHAKA na LILIAN JOEL




























