CHAMA Cha Wahasibu Tanzania (CPA) na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kusitisha ukusanyaji kodi za malimbikizo ya miaka zaidi ya mitano nyuma na kusema ulikuwa kifo cha mitaji ya wengi.
Pia, kupitia agizo hilo la Rais Samia, CPA na JWT wametangaza mkakati rasmi wa kukabiliana na wahasibu feki ‘vishoka’ wanaodaiwa kuhusika kuikosesha serikali mapato na kuwatia hasara wafanyabiashara.
Mkakaati huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, Juni 21 mwaka huu, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Hayo yamefikiwa katika kikao maalumu kilichowakutanisha viongozi wa CPA na JWT, kilichofanyika Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, lengo likiwa kuimarisha ushirikiano utakaosaidia wafanyabiashara kuwa na kumbukumbu nzuri na kuandaa vitabu vya mahesabu vizuri vitakavyoakisi uhalisia wa biashara zao.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa JWT, Hamis Livembe, alisema jumuiya inampongeza Rais Samia kwa tamko hilo na hatua alizochukua katika kusitisha ukusanyaji kodi ya miaka mitano nyuma.
“Katika jambo moja lililokuwa linachangia kuangusha mitaji ya wafanyabiashara ni hilo la ukusanyaji kodi za miaka mingi nyuma. Hili lilikuwa linawaumiza wafanyabiashara na kodi nyingi za aina hii zilikuwa za kuzusha,” alibainisha Livembe.
Alisema tamko hilo la Rais Samia limekuwa faraja kubwa kwa wafanyabiashara na kumuomba alisimamie katika utekelezaji wake.
“Wafanyabiashara tumelipokea vizuri na tunamuunga mkono Rais wetu. Baada ya tamko lile simu zimekuwa nyingi na kupitia katika mitandao yetu ya kijamii tumekuwa tukipokea pongezi zake kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali, kiasi kwamba mitandao imejaa,” alisema.
Alimuomba Rais Samia kusimamia tamko lake kwa sababu wapo baadhi ya watu waliokuwa wakinufaika na ukusanyaji wa kodi hizo za nyuma.
Kuhusu wahasibu vishoka, Livembe alisema kiasi kikubwa wafanyabiashara ni waathirika wa vishoka hao, kwa sababu ndio wanaohukumiwa kutokana na makosa ya kiuhasibu.
“Awali wafanyabiashara tulikuwa hatutambui kama kuna wahasibu vishoka. Katika kikao hiki tumekubaliana na CPA kuwa na mfumo maalumu wa kuwatambua wahasibu kuanzia ngazi za wilaya na mikoa,” alibainisha.
Kwa upande wake, Rais wa CPA, Godvictor Lyimo, alisema kikao hicho kiliitishwa kutokana na kuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu wahasibu vishoka.
“Wahasibu vishoka hawa wanachangia kuandaa vitabu vya hesabu, ambavyo siyo sahihi na kusababisha makadirio ya kodi ambayo pia yanakuwa siyo sahihi, hivyo kuchangia kuweka mianya ya rushwa na kuangamiza mitaji ya wafanyabiashara,” alieleza.
Lyimo alisema kutokana hali hiyo, Juni 21 mwaka huu, CPA itazindua mfumo maalumu wa kimtandao utakaomrahisishia mfanyabiashara kumtambua mhasibu sahihi, mahali alipo ambaye amesajiliwa na kutambulika na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Ukaguzi Tanzania (NBAA) ambaye anaweza kumsaidia.
Lyimo alisema hatua hiyo imechagizwa na agizo la Rais Samia, akiwa ziarani mkoani Kagera hivi karibuni, aliposimamisha ukusanyaji wa malimbikizo ya kodi ya kuanzia miaka mitano nyuma.
Kulingana na Lyimo, wamebaini tatizo la malimbikizo ya kodi linatokana na utitiri wa wahasibu vishoka, ambao wanashindwa kuandaa vitabu vya hesabu. “Unapozungumzia malimbikizo ya kodi safari inaanza katika uandaaji wa hesabu za wafanyabiashara.
Wafanyabiashara wanaposhindwa kuandaa mahesabu yao kwa wakati inasababisha ugumu kwa watoza kodi kufanya kazi yao vizuri,” alieleza.
Lyimo alibainisha agizo la Rais Samia limechangia kuwafumbua macho na kuandaliwa kwa kikao hicho ili wafanyanyabiashara katika siku zijazo wawe na ushirikiano wa karibu na CPA, hali itakayosaidia serikali kukusanya mapato na wafanyabiashara kupata faida.
Alibainisha kikao hicho kililenga pia kuweka misingi imara ya kuwakutanisha wafanyabiashara na wahasibu sahihi, ambao watawasaidia kuandaa vitabu vya mahesabu.
Juni 9, mwaka huu akiwa ziarani mkoani Kagera, Rais Samia, alipiga marufuku wafanyabiashara kutozwa kodi ya malimbikizo ya miaka zaidi ya mitano nyuma, isipokuwa kodi ya kuanza mwaka mmoja nyuma.
Na CHRISTOPHER LISSA