CHAMA cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), kimeipongeza Serikali kwa kuweka punguzo la tozo katika matumizi ya barabara, kutoka dola za Marekani 16 (sh. 37,328) hadi dola 10 (sh. 23,330) kwa kilomita 100, ikiwemo kuondoa kodi katika ‘matrela’ na vichwa vya magari ya kusafirishia mizigo.
Pia, kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza na kufanyia kazi changamoto za sekta ya usafirishaji, kupitia Bajeti Kuu yaSerikali ya Mwaka 2022/2023.
Akizungumza na UHURU, Rais wa TAT, Mohammed Abdullah, amesema punguzo hilo litachangia kukuza uchumi, kwani baadhi ya madereva kutoka nchi jirani wakipita na kusafirisha mizigo yao itaongeza fedha za kigeni.
“Tunashukuru sana kwa punguzo katika kodi ya ‘matrela’ na vichwa vya magari ya kusafirishia mizigo hadi asilimia 0 na punguzo katika tozo ya matumizi ya barabara kutoka dola za Marekani 16 kwa kilomita 100 hadi dola 10 kwa kilomita 100,” alisema.
Aidha, Abdullah alieleza mabadiliko hayo ya tozo yanatarajiwa kuanza Julai Mosi, mwaka huu.
Alisema ana imani serikali chini ya Rais Samia ni sikivu na itaendelea kutatua changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya usafirishaji.
Vilevile aliipongeza serikali kupitia wataalamu mbalimbali waliopo katika sekta ya usafirishaji kwa namna inavyowashirikisha vyema wadau wa sekta binafsi katika masuala mbalimbali ikiwemo bajeti na kodi.
“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kuwa sikivu kwa maombi ya wasafirishaji nchini na tuna imani kubwa changamoto ambazo hazijatatuliwa, zitafanyiwa marekebisho ili zilete tija katika sekta ya usafirishaji na nchi kwa ujumla,” alisema.
BAJETI KUU
Akisoma bajeti kuu ya serikali mwaka 2022/2023 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema katika sekta ya usafirishaji serikali imekamilisha ujenzi wa jumla ya kilomita 216.26 za barabara kuu, kilomita 34.8 za barabara za mikoani kwa kiwango cha lami.
Pia, Dk. Mwigulu alisema kilomita 307.41 za barabara za mikoa zilikarabatiwa kwa kiwango cha changarawe.
Aliongeza serikali imeanza ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje (Outer Ring Road) zenye kilomita 112.3 katika Jiji la Dodoma na kuendelea na upanuzi wa njia nane katika Barabara ya Kimara hadi Kibaha mkoani Pwani kwa kilomita 19.2.
Dk. Mwigulu alisema serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja ya Tanzanite jijini, Dar es Salaam, Kiyegeya Morogoro na Ruhuhu Ruvuma, huku akifafanua hatua hizo zinalenga kufungua uchumi na kurahisisha sekta ya usafirishaji.
Na IRENE MWASOMOLA