SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeshusha neema ya ujenzi wa shule mpya 214 za sekondari zitakazojengwa katika kata za majimbo yote ya uchaguzi nchini.
Katika kutekeleza ujenzi huo, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imepeleka sh. bilioni 100.58 kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo.
Aidha, imetoa sh. bilioni 30 kujenga shule mpya za sekondari za wasichana katika mikoa 10 ya Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Desemba 4, 2021 na Ofisi ya Rais TAMISEMI, fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa SEQUIP.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, mradi huo unatekelezwa katika eneo la elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi sita kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 – 2024/2025.
Ilisema utekelezaji wa mradi huo, umeelekezwa katika maeneo ya vipaumbele vya serikali yanayogusa moja kwa moja elimu ya sekondari ambayo ni ujenzi wa shule mpya za sekondari 1,000.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shule hizo zitajengwa katika kata ambazo hazina shule za sekondari na maeneo ambayo yana wanafunzi wengi, ukilinganisha na miundombinu.
Pia, mradi huo utahusisha ujenzi wa shule mpya za sekondari za wasichana za mikoa 26, katika kila mkoa, itajengewa shule moja.
“Ujenzi wa shule hizi, utakua unafanyika kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana, kwa sasa tunaendelea na uchambuzi ili kujenga shule za nyongeza 20 katika kata zenye msongamano wa wanafunzi.
“Gharama ya ujenzi wa shule za sekondari za kata ni sh. milioni 600 kwa kila shule, kiasi kilichopelekwa katika awamu ya kwanza ni sh. milioni 470,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kuhusu gharama ya ujenzi wa shule za sekondari za wasichana za mikoa, taarifa hiyo iliweka wazi kwamba, itakuwa sh. bilioni nne, ambapo sh. bilioni tatu, zimetolewa ikiwa ni malipo ya awamu ya kwanza ya ujenzi kwa kila shule.
Ilifafanua kuwa, shule za sekondari za kata, zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wasiopungua 400 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, shule za wasichana za mikoa zitachukua wanafunzi wasiopungua 1,000 kwa kila shule.
“Mradi huu wa SEQUIP umelenga kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu ya sekondari, kuweka mazingira salama ya elimu kwa wasichana na kuhakikisha wanafunzi wote wanapata elimu bora ya sekondari,” alieleza.
Kufuatia upelekaji wa fedha hizo, Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu alitoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri, kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na serikali.
Katika maelekezo hayo, halmashauri zote zimetakiwa kuhakikisha maeneo yaliyoteuliwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo, hayana migogoro ya umiliki wa ardhi.
Pia, Halmashauri za Majiji na Manispaa ambazo zina ufinyu wa maeneo ya ujenzi, wanaruhusiwa kutumia ramani za ujenzi wa ghorofa ambapo halmashauri husika, zinatakiwa kuomba kibali cha kutumia kiasi kilichotengwa na mapato ya ndani kuweza kukamilisha ujenzi wa shule husika.
Aidha, kazi za ujenzi zimetakiwa kuanza ndani ya wiki mbili baada ya kupokea fedha na muongozo wa ujenzi na kukamilika katika kipindi cha miezi sita kwa shule za sekondari za kata na mwaka mmoja kwa shule za sekondari za mikoa.
Kadhalika, halmashauri zimetakiwa kuzingatia utaratibu wa usimamizi wa mazingira na ushirikishwaji wa jamii husika kabla, wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi kukamilika ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kama ukataji miti hovyo, uchafuzi wa mazingira na unyanyasaji wa kijinsia.
Maelekezo mengine ni kwamba, mradi huo unaweza kutekelezwa kwa kutumia utaratibu wa “force account” au wakandarasi na gharama za ujenzi kwa kutumia njia yoyote, zisizidi fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli husika.
Mradi wa SEQUIP, unatekelezwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ukilenga kuboresha elimu ya sekondari nchini.
Mradi huo, unagharamiwa na serikali kwa mkopo wa sh. trilioni 1.1 kutoka Benki ya Dunia.
NA MUSSA YUSUPH, DODOMA



























