RAIS Samia Suluhu Hassan, amewaongoza Watanzania kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru, huku akisema moja ya mafanikio ni kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na nchi zingine za Afrika.
Alisema uwepo wa viongozi wakuu wa nchi kadhaa hususan za Afrika ni ishara kuwa diplomasia imeimarika.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni Rais wa Kenya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) Uhuru Kenyatta, Rais wa Commoro, Azali Asoumani, Rais wa Msumbiji Felipe Nyusi na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema kuhudhuria kwa viongozi hao kutoka mataifa mengine ya Afrika, kunaonyesha mshikamano na umoja wa kanda za nchi hizo.
“Huu ndio umoja wa Afrika miaka 60 ya mafanikio ni pamoja na kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika,”alisema.
Katika utambulisho wake, Rais Samia alimtambilisha Rais Uhuru Kenyatta kuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo na kuwa amekuja kwa ziara maalumu ya siku mbili.
“Huyu mgeni rasmi kwa kuwa amekuja kwa ziara maalumu na ukizingatia kule kwake kuna vuguvugu la uchaguzi kwa hiyo hii ni mara ya mwisho tunamualika kama Rais awamu nyingine huenda akawa mstaafu,” alisema.
Alitaja mataifa mengine yaliyohudhuria yakiwakilishwa na viongozi mbalimbali ni Burundi, Eswatini, Oman, Uganda, Afrika Kusini, Zimbabwe, Kuwait na Namibia.
Rais Samia alisema mbali na wakuu wa nchi waliohudhuria sherehe hizo pia walikuwepo wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kimtaifa ikiwemo Umoja wa Afrika, mabalozi wa Tanzania na wanaoziwakilisha nchi zao nchini.
Aliongeza kuwa: “Wengine waliohudhuria ni viongozi wa vyama vya siasa wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo na wanasiasa wengine wakiwemo wabunge wa Tanzania.”
Rais Samia alitumia fursa hiyo kusifu uzalendo wa watanzania katika maadhimisho hayo.
Kwa upande wake,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema hotuba ya Rais juzi imekuwa chachu ya kuimarika kwa amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.
Aliongeza kuwa hotuba hiyo, inawakumbusha watanzania wajibu wa kutafakari taifa lilipotoka, lilipo na linapokwenda.
Majaliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi wa sherehe hizo, alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa maelekezo na miongozo iliyofanikisha maandalizi, kamati ya kitaifa iliyohusisha wajumbe kutoka Bara na Zanzibar na wananchi kwa ujumla.
Alisema hatua hiyo imedhihirisha umoja na mshikamano uliopo kwa Watanzania.
Mariam Mziwanda na Juma Is’haka



























