RAIS Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa wakurugenzi wanne wa Halmashauri za Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Manispaa ya Iringa, Singida na Jiji la Mbeya kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za umma zikiwemo za UVIKO-19.
Pia, amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kuunda Tume ya kuchunguza Jeshi la Polisi kuhusiana na tuhuma za mauaji ya mfanyabishara wa madini Mussa Hamis (25) aliayeuawa hivi karibuni mkoani Mtwara.
Rais Samia pia amewataka wananchi kuachana na maneno maneno ya baadhi ya watu wanaopotosha kuwa mpango wa Elimu Bure umefutwa na miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Hayati Dk. John Magufuli ikiwemo ya kimkakati, haitakamilika.
Amesema na kutoa maagizo hayo mjini Magu wakati akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kumpokea na kumsikiliza wakati akielekea mkoani Mara kwenye maadhimishao ya miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Samia ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa Machifu (Chifu Hangaya), ametoa maagizo hayo kufuatia taarifa ya Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa, kutoa salamu kwa wananchi na kueleza kuwa Wizara yake inafanya uchunguzi wa ubadhilifu wa fedha za UVIKO-19 katika Halmashauri ya Buchosa, Iringa, Singida na Mbeya ambayo mapato ya nusu mwaka yameshuka kuliko kawaida baada mashine za kukusanyia mapato (Poss) zaidi ya 72 kuzimwa kwa zaidi ya siku 100.
Bashungwa pia ameitaja Halmashauri nyingine inayochunguzwa kuwa ni ya Geita Vijijini ambako Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Msukuma, alidai kuna ubadhilifu katika halamashauri hiyo.
Kufuatia taarifa ya Bashungwa, Rais Samia amesema alishatoa maagizo na kuonya mapema kuwa mtu yeyote asichezee fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi na Mapambano ya UVIKO-19.
“Waziri nilisema Mkurugenzi atakayetaka kuijua rangi yangu achezee fedha hizo na kwa taarifa zilizopo wakurugenzi wa Buchosa, Iringa, Mbeya na Singida Mjini, wakurugenzi wamechezea fedha hizo, kuanzia sasa hivi wakurugenzi hao nimewatengua,”
“Nimewatengua sasa hivi na baadae nitaona ripoti yako inasemaje maana mna kawaida ya kuwafichiafichia lakini nina ripoti kabla ya kwenu,” alisema Rais Samia huku akisisitiza kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita mjini uchunguzi uendelee, ikithibitika naye ana makosa kama hayo, atatumbuliwa pia.
Wakurugenzi waliotumbuliwa ni Paul Malaga (Buchosa), Amnede Ng’wanidako (Jiji Mbeya), Benard Limbe (Manispaa Iringa), Zefrin Lubuva (Manispaa ya Singida) na John Wanga wa Buchosa ambaye anaeendelea kuchunguzwa.
Akizungumzia matukio ya mauji yaliyoshamiri hivi karibuni nchini likiwemo lile la Polisi mkoani Mtwara kumuua mfanyabiashara huyo mkazi wa Kijiji cha Luponda Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Rais amesema haiwezekani jeshi la polisi lifanye mauaji halafu lijichunguze lenyewe.
Amesema hayo baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masaun, kuelezea baadhi ya maauaji yaliyolikumba taifa yakiwemo ya Mwanza .
Waziri Masaun amesema Jeshi la polisi liko imara kushughulikia matukio ya uhalifu yakiwemo ya mauaji manne yaliyotokea mkoani Mwanza ambayo tayari watuhumiwa wameisha tiwa mbaroni.
Aidha, Rais amemueleza Masaun kuwa anataka Polisi ijitafakari kama linavyofanya ndiyo misingi yake au vinginevyo na kwamba taarifa ya kamati huru itakayoundwa na Waziri Mkuu itakapopelekwa italinganishwa na ile ya Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe.
NA PETER KATULANDA. Magu