RAIS Samia Suluhu Hassan, ameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kuzingatia maeneo manne katika utekelezaji madhubuti wa dhamira ya mageuzi ya mfumo wa sekta ya elimu.
Ametaja maeneo hayo ni mitaala ya kufundishia, ukaguzi wa elimu, utungaji mitihani na sifa za walimu. Rais Samia alitoa kauli hiyo, wakati akizindua Taasisi ya Mwanamke ‘Initiative Foundation’ Mkoa wa Mjini Magharibi na kusisitiza kuhusu umuhimu wa kuwepo taasisi na watu watakaoisaidia serikali kutatua changamoto za sekta ya elimu.
Alisema changamoto za miundombinu ya elimu na mafunzo yanayotolewa ikiwemo mitaala, inahitaji kufanyiwa mtazamo mpya na amefarijika kusikia ahadi ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhusu kufanya mageuzi ya elimu.
“Lakini na mimi nataka kutoa mchango wangu hapa, mtakapokwenda kuanza hayo mageuzi naomba sana muangalie maeneo yafuatayo; la kwanza mitaala na la pili ni wakaguzi wa elimu, naomba muangalie utendaji wao, sifa zao na kuwawezesha vitendea kazi ili waweze kuzunguka na kufanya ukaguzi kama unavyotakiwa,” alisema.
Rais Samia alieleza wakaguzi hao wanatakiwa wasiwe wakaguzi majina tu, lakini wawe wakaguzi wenye sifa na jambo lingine ni utungaji mitihani na namna ya ufundishaji watoto.
“Mbali na hilo, jambo lingine ni sifa za walimu amesema hapa mtendaji mkuu wa taasisi, kwamba katika majaribio yao ya kuangalia uwezo wa walimu, mwalimu mkuu hakumbuki amefaulisha wanafunzi wangapi kwa hiyo muangalie sifa za walimu,” alisema.
Rais Samia alisema amefurahishwa na jambo la walimu wa kujitolea ambao ni wahitimu waliotoka chuo wanaosubiri ajira.
ARIDHISWA NA MIPANGO YA SMZ
Rais Samia alisema ameridhishwa na maelezo ya serikali ya Zanzibar, kuhusu mabadiliko makubwa yaliyopangwa katika kukabiliana na changamoto za elimu na kubainisha uboreshaji mitaala ya kufundishia utatoa elimu yenye tija zaidi.
“Kuweka kipaumbele katika mafunzo ya amali na kudhamiria kujenga shule 10 za mafunzo ya amali, kuongeza shule za ufundi kila wilaya na kuongeza ajira zaidi ya 4,000 kwa mwaka wa fedha 2022/2023, hizi ni hatua kubwa sana,” alisema Rais Samia.
Aliongeza: “Hizi ni hatua ambazo zinaleta matumaini kwamba, mbele ya safari kutakuwa na mwanga na katika ajira hizo 4,000 za walimu, tunapaswa kuwaajiri walimu wenye sifa.”
ATOA MAPENDEKEZO KWA SMZ
Rais Samia alipendekeza katika ajira na mikataba ya vipindi vifupi, kipaumbele kiwe kwa walimu walioanza kujitolea kwa sababu wameonyesha uwezo wao kazini bila kuajiriwa.
“Pendekezo langu ni kuwa walimu mkiwasainisha mkataba kwamba huyu ana ajira ya maisha, hatakuwa na haja ya kujihangaisha akaongeze uwezo wake wa kufanya kazi kwa sababu anajua atakwenda shule kuuza visheti, kufundisha mtoto na mshahara wake bado upo.
“Lakini walimu hao wakiwekewa vipindi vya mikataba, walimu watajituma na kweli wakapimwa na wasiofanya vizuri wakatolewa, ni imani yangu walimu watafanya kazi.
“Kadhalika tunavyokwenda hivi tukishasaini mkataba wa kazi mpaka astaafu, walimu hawatajituma naombeni sana, muweke vipimo vya upimaji wa kazi za walimu na kweli vifanye kazi, watoto wetu watafundishwa vizuri,” alisema Rais Samia.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, anaunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na taasisi hiyo, hasa kwa upande wa Zanzibar.
Alisema SMZ itaendelea kutoa ushirikiano kwa kipindi chote na atahakikisha shughuli zote zinazotakiwa kusimamiwa, serikali itazisimamia na kuunga mkono juhudi hizo.
“Mimi nimekuwa shuhuda mkubwa sana wa taasisi hii, mnamo Juni 4, mwaka huu, walinialika na zaidi ya sh. milioni 116 na vifaa mbalimbali vilikabidhiwa kwa Mkoa wa Kusini Unguja na mimi ndiyo nilivikabidhi,” alisema.
Alifafanua vifaa hivyo alivyokabidhi vinatokana na mafanikio makubwa ya taasisi hiyo kuanzisha mpango wa kusaidia sekta ya elimu Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais alieleza mwaka 2020 katika Mkoa wa Kusini Unguja kulingana na takwimu za matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, kulikuwa na ufaulu wa asilimia 50, lakini matokeo ya mwaka 2021 katika mkoa huo, kiwango cha ufaulu kilipanda hadi asilimia 72.
Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa, alisema taasisi hiyo inasaidia serikali kuwafi kia watu wengi wanaotaka waingie katika shughuli za elimu.
“Hivyo ninapongeza taasisi hii na kuahidi kufanya nayo kazi vizuri ili kuhakikisha lengo la kuanzishwa kwa taasisi ya MIF linafi kiwa kwa walengwa wote,” alisema.
Vilevile, Waziri Ofi si ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Muhagama, alisema kwa miaka 60 ya Uhuru, Tanzania imeonyesha wanawake ni watu muhimu katika ustawi wa taifa kama ambavyo Rais Samia anavyozidi kuonyesha ujasiri wake katika uongozi.
Alisema MIF ikisimama vizuri na kuwezesha watoto wa kike, tafsiri yake inaandaa viongozi wakubwa wa baadaye watakaofanya mageuzi ya maendeleo nchini.
“Ni kitu fulani ambacho tunatakiwa kujifunza kama wanawake kupitia kwanza kwa Rais Samia, lakini sisi kama wanawake ni lazima tujipange sawasawa kuuonyesha ulimwengu Mwenyezi Mungu hakukosea kutuumba wanawake, lakini ana sababu za msingi ndani yetu katika kusaidia sekta mbalimbali katika ulimwengu,” alisema.
Waziri Jenista aliwataka wanawake kumuunga mkono Rais Samia kwa kuhakikisha wanashirikiana kwa lengo la kuleta ustawi wa taifa.
Akitoa maelezo kuhusu Taasisi ya Mwanamke ‘Initiatives Foundation’ (MIF), Mtendaji Mkuu Fatma Mwasa, alisema IMF ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Alisema taasisi hiyo ipo kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika jamii na lengo ni kuwasaidia vijana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 28.
Alisema mtazamo wao ni kuona wanakuwa na jamii huru iliyo na maendeleo, lakini haisumbuliwi na umasikini, ujinga na maradhi na mipango ya taasisi hiyo ni kuendesha shughuli kimkakati wakiunganisha nguvu na taasisi nyingine katika kufi kia malengo.
Fatma alisema taasisi ya MIF inaendesha shughuli kwa kutazama malengo makubwa manne, ikiwemo kumuinua mtoto wa kike kielimu na kuwezesha vijana kiuchumi.
Alitaja malengo mengine ya IMF ni kujenga uelewa kuhusu afya ya akili na kushughulika na afya ya uzazi kwa vijana.
HANIFA RAMADHANI Na EMMANUEL MOHAMED, Zanzibar