SIKU moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutoa maelekezo kwa Tume ya Utumishi wa Umma, kuhusu nidhamu kwa watumishi, wasomi na viongozi wa dini wametoa maoni tofauti.
Katika maelekezo yake, Rais Samia alitoa maagizo manne kwa Tume ya Utumishi wa Umma, huku akionya kutetereka kwa nidhamu kwa watumishi wa umma nchini.
Rais Samia alitoa kauli hiyo, Mei 21, 2022, Ikulu Chamwino, jijini Dodoma, wakati akiwaapisha manaibu katibu wakuu na makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma.
Kwa mujibu wa Rais Samia nidhamu katika utumishi wa umma imetetereka, kwa sababu kwa muda mrefu hakuna mafunzo mbalimbali kwa kada za utumishi wa umma.
Wakiizungumzia kauli ya Rais Samia, baadhi ya wasomi na viongozi wa dini wamesema wanaiunga mkono kwa kuwa imelenga kuboresha utendaji sehemu ya kazi.
Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Lwoga, amesema ili kupata watumishi bora, ni vyema mfumo wa elimu ukaboreshwa ili kupata watumishi watakaotimiza wajibu wao kazini.
“Ni vizuri kukawa na semina za mara kwa kwa watumishi na viongozi ili wakumbushwe wajibu wao wa kuwatumikia wananchi,” alisema Profesa Lwoga.
Naye Dokta Imelda Gervas, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), amewataka watumishi kutambua sababu za wao kupata nafasi za kuwatumikia wananchi.
Dk. Imelda amepongeza kauli ya Rais Samia aliyotoa kwa watumishi wa umma, akisema kuwa ana matumaini itawarejesha katika mstari watumishi wazembe.
Amesema tamko la Rais Samia limekuja wakati mwafaka, baada ya hivi karibuni kuibuka malalamiko kwa baadhi ya watumishi wa umma kukosa maadili ya kazi.
“Tunahitaji kujenga msingi wa maisha ya watumishi kupitia elimu, lakini hata viongozi katika ofisi lazima wawe na tabia ya kuzungumza na watendaji ili iwasaidie kujua matatizo yao,” alisema.
Askofu wa Kanisani la Ligth House Christian Center (LHCC), Profesa Rejoice Ndalima, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Jumuiya ya Madaktari na Maprofesa wa Falsafa nchini (APDPT), amesema suala la maadili ni muhimu kwa watumishi wa umma.
ProfesaNdalima amesema maadili ni jambo la msingi na ameishauri serikali kurejesha elimu ya uzalendo na maadili kuanzia ya awali, msingi, sekondari na vyuo kikuu ili kujenga nidhamu ya utendaji.
“Viongozi warejee katika maadili na mafundisho ya dini yatakayowajengea hofu ya kufanya vitu vilivyo kinyume na uzalendo na maadili,” amesema Profesa Ndalima.
Aidha, amesema viongozi wanaoteuliwa wafanyekazi kwa uadilifu na uzalendo ili kumsaidia Rais Samia na wasifanye kazi kwa kutaka kuonekana.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hery Mkunda, amesema hakuna haki bila ya kutekeleza wajibu wa kazi vizuri.
Amesema kila mfanyakazi anapaswa kufanya kazi ili kutimiza wajibu wake sehemu ya kazi kama sheria ya kazi inavyomuongoza.
“Sisi hatulei wafanyakazi wezi, wazembe, wavivu na wabadhilifu ila tunawalea wafanyakazi wanaotekeleza wajibu wao wa kazi,”amesema Mkunda.
Mkunda ameongeza kuwa, Rais ametimiza wajibu wake unaostahili kwa sababu yeye ameshatimiza haki yake kwa wafanyakazi wa kuwaongezea nyongeza ya aslimia 23.3 ya mshahara wao, hivyo ongezeko hilo linatakiwa lifanyiwe kazi ili Watanzania wapate kile wanachostahili.
“Watanzania wanatakiwa kutendewa haki zao za msingi, ikiwemo kupata huduma bora kutoka kwa waowajibika kutoa huduma hiyo,”amesema.
Mkunda amesema TUCTA ipo kwa ajili ya kuwahimiza wafanyakazi wafanye kazi kwa bidii na kuangalia maslahi yao hasa pale wanapofanya kazi vizuri.
Naye, Mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sylvester Rugeihyamu, alisema uwajibikaji wa kazi ni msingi mzuri ambao unaleta maendeleo sehemu ya kazi.
“Si kila kitu mkuu wa nchi aseme na ukiona amesema ujue kuna uzembe umefanyika ngazi ya juu, umesababisha uwajibikaji kuwa mdogo kwa watendaji wa kawaida,” alisema Dk. Rugeihyamu.
Dk. Rugeiyamu alisema Tanzania inaelekea kupata wageni wengi kutoka nchi za nje kama wawekezaji hivyo watumishi wa umma wanatakiwa kuwa makini katika utoaji wa huduma zao.
“Sekta ya afya na Uhamiaji ni sehemu ambayo itakuwa inapokea wageni wengi wanaohitaji huduma sasa ikiwa hadi mkuu wa nchi azungumze ndio watu wafanyekazi moja kwa moja tunakwenda kuzorotesha juhudi zinazofanywa na Rais Samia,” alisema.
Kwa upande wake, Mchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Timoth Lyanga, alisema kila mfanyakazi anatakiwa kuwajibika sehemu yake ya kazi.
Dk. Lyanga alisema uwabikaji uanzie kwa viongozi wa juu na watendaji wa chini watafanya vizuri shughuli zao za kiutendaji.
“Haipendezi kila kitu kiongozi wa juu azumze, ikiwa mtu unapokea mshahara wako na haki zako zote ni vyema ukatimiza wajibu wako unaotakiwa,”alisema.
Katibu wa Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) Taifa, Sheikh Hassan Chizenga, amempongeza Rais Samia kwa kuona changamoto hiyo ya mmonyoko wa maadili katika utumishi wa umma na kusema kwa kuliona hilo itakuwa ni njia ya kulitatua.
Sheikh Chizenga alisema maadili ni muhimu na yana sehemu kubwa katika utumishi wa umma, hivyo yanatakiwa kuzingatiwa ipasavyo.
“Njia ya kujenga maadili kwa jamii na viongozi ni kuweka mkazo kwa masomo ya dini, yapewe nafasi zaidi kama yalivyo masomo mengine, badala ya kufundisha siku moja,” alifafanua Sheikh Chizenga.
Alisema changamoto ya sasa iliyopo katika jamii inayopelekea mmomonyoko wa maadili zaidi ni utandawazi, hivyo njia bora ni kufundisha masomo ya dini katika vyuo na mafunzo mbalimbali ya taaluma, ikiwemo jeshi, udakatari, walimu na mengine.
NA WAANDISHI WETU