RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itahakikisha inamaliza na kufungua miradi yote ya barabara iliyomalizika kujengwa nchi nzima kwa kuwa nia na dhamira yake ni kuhakikisha anaifungua nchi kupitia miundombinu ya barabara.
Pia, ameitaka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuhakikisha inatangaza fedha za miradi ya afya na maji katika fedha za Uviko-19 zilizotolewa na Serikali katika halmashauri nchini.
Aliyasema hayo katika Kijiji cha Tura, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, wakati wa ufunguzi wa barabara ya Tabora- Nyahua- Chaya yenye urefu wa kilometa 170, ambapo Rais Samia, alifungua sehemu ya Nyahua hadi Chaya yenye urefu wa kilometa 85.4.
Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, ni sehemu ya barabara ya Tabora hadi Manyoni mkoani Singida, ambayo inaunganisha ukanda wa kati kuanzia Manyoni kupitia Tabora, Kigoma na Katavi.
Sehemu ya Barabara ya Nyahua hadi Chaya, imejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 117.9 ikiwa imegharamiwa na Serikali kwa asilimia 28 huku Kuwait ikiigharamia barabara hiyo kwa asilimia 72 kupitia fedha walizotoa za ujenzi wa sehemu hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia amesema amedhamiria kuufanya Mkoa wa Tabora kuwa na barabara za lami kwa sababu anapofungua barabara hiyo, anakumbuka historia kubwa kuhusu mkoa huo kichwani kwake.
Rais Samia alisema wakati akiwa mbunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge wa Urambo, Margareth Sitta, alikuwa analalamika ukosefu wa barabara za lami mkoani humo, pamoja na mkoa huo kuwa chachu ya kupigania Uhuru wa Tanzania.
“Nafarijika sana ninapofungua barabara hii, nakumbuka dada yangu Mama Sitta aliwahi kulalamika bungeni. Sasa namwambia serikali ya awamu ya sita italimaliza hilo na kuuhakikisha mkoa mzima unakuwa na barabara za lami,” alisema.
Alisema ufunguzi wa barabara hiyo ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuhakikisha inazifungua barabara zote zilizojengwa na kuzimalizia zile ambazo bado hazijamalizika kwa kuwa, nia na malengo ni kuifanya nchi inafunguka kupitia barabara.
“Barabara hii ni muhimu sana kwa kuwa ni kuu inayounganisha Tabora na mikoa mingine ikiwemo Singida, Kigoma, Katavi na nchi jirani za DRC na Burundi.
“Hivyo, kumalizika kwa kipande hicho ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa nchi,” alisema.
Alisema barabara hiyo, itarahisisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani kupitia Bandari ya Dar es Salaam, hivyo kumalizika kwa barabara ni moja ya mipango bora ya Serikali kuwa na miundombinu ya uhakika.
Rais Samia alisema anatambua kuna miradi mingi ya barabara imemalizika, inasubiri kufunguliwa, hivyo anawaahidi Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS), Watanzania wote kuwa, miradi hiyo ataifungua ili kuwaonyesha wapinga maendeleo juhudi za serikali katika ujenzi wa miundombinu.
“Naishukuru sana Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait kwa kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo, anaahidi ushirikiano wa dhati na nchi ya Kuwait na Tanzania itaendelea kudumisha uhusiano na umoja uliopo,” alisema.
Aliongeza ”Nawapongeza TANROADS kwa usimamizi wa mradi huu, wakandarasi na wafanyakazi kwa kuhakikisha unamalizika kwa wakati na umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi”.

MBARAWA
Awali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha wanatekeleza miradi yote iliyopo kwa kuhakikisha inamalizika kwa wakati.
“Tunakupongeza Rais Samia kwa juhudi zako za kuhakikisha kila siku miradi ya barabara inajengwa na kumalizika ili kuifungua nchi, akiwa kama Waziri, atahakikisha anazitaka taasisi zote zilizo chini yake, kuhakikisha wanamaliza miundombinu wanayoisimamia” alisema.
KAKOSO
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Kakoso, alisema amekuwa akipita maeneo mbalimbali ya nchi na kushuhudia mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya sita katika kutekeleza miradi ya miundombinu kwa kasi kubwa.
“Wanaosema hakuna miradi inayoendelea nchini, wanadanganya na wanapaswa kukemewa, Rais Samia unafanya kazi kubwa ya ujenzi wa miradi ya miundombinu, hilo sisi kama Bunge, tumeliona katika ziara zetu tunazofanya maeneo mbalimbali ya nchi,” alisema.
MTENDAJI TANROADS
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila, alisema ufunguzi wa barabara hiyo, una manufaa makubwa kwa nchi kwa kuwa, barabara hiyo ni muhimu katika kuinganisha nchi na zile za jirani katika ufanyaji biashara.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait, Waleed Albahar, alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake na kumwahidi nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi.
MAAGIZO TAMISEMI
Katika ufunguzi huo wa barabara, Rais Samia alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, kuhakikisha wizara inatangaza zabuni ya ununuzi wa vifaa mbalimbali kutoka nje kwa wakati.
“Tulipata fedha za Uviko-19 na kuzigawanya katika mikoa kwamba, ndani ya kipindi cha miezi tisa, ziwe zimefanyiwa kazi.
“Nina taarifa kuna ucheleweshwaji wa utangazaji zabuni katika miradi ya afya na maji. Waziri uko hapa, waeleze wenzako juu ya hilo,”alisema.
Alisema ucheleweshwaji wa kutangazwa zabuni kupitia fedha hizo, una athari kubwa kwa nchi, hususan wakati huu ambao Tanzania inatarajia kupokea fedha zingine.
Rais Samia alisema ni wakati wa wizara kuhakikisha inatangaza zabuni hizo haraka huku akizionya halmashauri kutumia vyema fedha za serikali zinazopelekwa katika wilaya zao.
CHANGAMOTO TABORA
Rais Samia alisema anazifahamu changamoto za Tabora likiwemo suala la ukubwa wa maeneo wilayani Uyui, uhaba wa watumishi wa kada mbalimbali kama walimu wa shule za msingi hasa masomo ya sayansi, wauguzi n.k.
“Nawaahidi changamoto zote nitazitatua ikiwemo kumaliza au kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi, lakini pia naziomba Halmashauri nazo kuhakikisha inatatua zingine na isisubiri serikali kuu pekee, wanapaswa kuanza wao kabla ya kuja serikali kuu,” alisema.
Akizungumzia suala la kuugawa wilaya ya Uyui, alisema kwa sasa ni mapema na malengo yake ni kujenga uchumi wa nchi.
RC TABORA
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk. Batilda Buriani, amempongeza Rais Samia kwa kufanya kazi kubwa katika kipindi chake cha mwaka mmoja na mafanikio yameonekana.
Hamis Shimye na Allan Kitwe, Tabora