Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan ametoa tuzo maalum kwa Benki ya NMB katika kutambua mchango na utendaji mzuri wa taasisi hiyo ya fedha nchini.
Akizungumza katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma kinachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa AICC jijini Arusha, Rais Samia amesema pamoja na kuwapongeza wale waliofanya vizuri, serikali pia itafanya tathmini ya utendaji wa taasisi na mashirika mengine nchini.
“Kupitia mashirika, serikali inaweza kukusanya fedha nyingi za kutosha kujazia upungufu wa bajeti ya nchi na hivyo kuipunguzia serikali mzigo wa kwenda kukopa nje,” alisema Dkt. Samia.
“Ni muhimu sana ofisi ya msajili wa hazina ihakikishe inasimamia ipasavyo sheria na kanuni zilizopo katika kuhakikisha kuwa taasisi za umma zinajiendesha kwa tija na kuipunguzia serikali mzigo wa gharama za kuziendesha,” alisema Rais Samia.
Pamoja na kutoa pongezi kwa Benki ya NMB, Rais Samia pia amemkabidhi cheti cha mlipa gawio kubwa serikalini katika sekta ya kibenki, Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo ya fedha Ruth Zaipuna.
Benki ya NMB imetoa gawio la shilingi Billioni 45.5 serikalini katika mwaka wa fedha uliopita.
Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, Nehemiah Kyando Mchechu, Serikali inamiliki asilimia 31.8 ya hisa katika benki ya NMB.
“Tumetoa tuzo kwa taasisi zilizofanya vizuri ili kuleta changamoto katika kujifunza sisi sote na ili taasisi zingine ziwe na wivu wa kusonga mbele ndio tuweze kuisaidia nchi yetu,” alisema Mchechu.
Kwa mujibu wa Msajili huyo wa Hazina, serikali imewekeza zaidi ya shilingi trillioni 73 katika taasisi za umma na kwamba ni jukumu lao kuhakikisha fedha hizo zinazaa matunda makubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
“Tunatarajia kuwa siku za mbeleni pamoja na kuwa na list of fame (orodha ya sifa), ya taasisi zinazofanya vizuri, baadae pia tungeweza kuwa na list of shame (ordha ya aibu) kwa taasisi zinazofanya vibaya lakini hatutarajii kufika huko, kutokana na maboresho makubwa tunayofanya kwa taasisi hizi kwa sasa,” alisema Mchechu.
Jumla ya taasisi 248 zimeshiriki mkutano huo wa kwanza wa mwaka wa kikao Kazi cha wenyekiti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma ukiwa na washiriki Zaidi ya 600.