RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Mhandisi Patrick Mfugale, atakumbukwa kwa utendaji uliotukuka na ameacha alama kubwa nchini.
Rais Samia ameyasema hayo leo (Julai 02, 2021), wakati akiongoza Watanzania kumuaga aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Amesema miongoni mwa alama hizo ni ujenzi wa barabara na madaraja likiwemo la JP Magufuli, ambalo amefariki kabla ya kutimiza dhamira yake ya kulikamilisha.
Ameeleza kuwa kiongozi huyo, ametumikia TANROADS kwa takribani miaka 12 na kufafanua kuwa siri ya kuaminiwa kwake na awamu mbalimbali za serikali ni ufanisi wake.
“Familia imempoteza mtu muhimu waliompenda na kumtegemea, serikali imepoteza mtumishi na kiongozi mwadilifu, makini shupavu na mchapakazi hodari na taifa limepoteza Mhandisi mahiri na mzalendo wa kweli aliyekuwa tayari kuitumikia nchi kwa moyo wake wote ” amesema.
Amefafanua kuwa kwa mara ya mwisho alionana na Mhandisi Mfugale, mwezi Juni alipofanya ziara ya kukagua Daraja la JP Magufuli jijini Mwanza.
“Siku hiyo alionekana makini na alinipa maelezo ya kina kuhusu daraja lile na matumaini yake jinsi ya kulijenga na kulikamilisha bahati mbaya tunachopanga wanadamu Mungu hapangi hicho, amemchukua kabla ya matumaini yake kutimia,” amesema.
Aliongeza Mhandisi Mfugale alikuwa mjumbe wa timu za wataalamu wa serikali katika miradi ya kimkakati likiwemo Bwawa la Umeme la Julius Nyerere na hadi umauti unamkuta alikuwa tayari amekamilisha michoro ya barabara za mzunguko na njia nne Dodoma.
“Kifo chake kibaki kama funzo kwa watanzania kwamba atakayebahatika kupata umri duniani lazima aache alama, leo tunamzungumza Mfugale kwa yote haya nasi hatuna budi kufuata nyendo zake na kujitahidi kuacha alama popote na katika nafasi yoyote tutakayokuwa,” amesisitiza.
Amesema iwapo kila mtu ataishi maisha ya kutumia kipaji alichopewa kuacha alama, Tanzania itapata maendeleo ya haraka.
Akitoa taarifa ya mwisho kabla ya kifo chake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, amesema Mhandisi Mfugale alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Amebainisha kabla ya umauti walipanga kukutana kwa kikao cha Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na TANROADS kilichopangwa kufanyika ijumaa (Juni 25, mwaka huu) lakini Mhandisi Mfugale aliomba kiahirishwe na kifanyike Juni 29, kwa kile alichosema kuwa alikuwa na jukumu ambalo asingeweza kuliahirisha.
“Kama ulivyo utaratibu wa Wizara yetu, tukakubali ombi lake na kupanga kikao kifanyike Jumanne (Juni 29, mwaka huu) jijini Dodoma,” ameeleza.
Amefafanua kuwa siku ya kikao ilipofika yeye alikwenda bungeni na kuwakilishwa na Katibu Mkuu Ujenzi, Mhandisi Joseph Malongo, hivyo kilianza saa nne asubuhi.
Kwa mujibu wa Dk. Chamuriho, kabla ya kikao Mhandisi Mfugale alieleza kuwa anajisikia vibaya hivyo alikwenda kukaa ofisi ya Katibu Mkuu huyo kwa mapumziko, huku kikao kikiendelea.
Amesema baadaye Mhandisi Malongo alitoka katika kikao na kwenda kumuangalia Mhandisi Mfugale na alimkuta amekaa katika kiti huku hali yake ikionekana kutokuwa shwari.
“Alipomkuta katika hali hiyo aliwauliza waliokuwa karibu na ofisi ile walimwambia alipoingia aliomba kuongezewa kioyozi ili apate hewa,” amebanisha.
Baada ya hali hiyo, amesema ulifanywa mchakato wa kuita gari na kumkimbiza Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma na alipofikishwa uchunguzi wa kina wa madaktari ulibainisha kuwa alishafariki.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Crispianus Ako, amesema Mhandisi Mfugale aliingia katika wakala huo mwaka 2010 akiwa Mtendaji Mkuu wan ne tangu ulipoanzishwa.
Amesema uongozi wake ndiyo uliobadili taswira ya taasisi kutoka kusemwa vibaya na vyombo vya habari hadi kusifiwa, kwa kuwa aliwafundisha watumishi kufanya kazi na aliwataka kila mmoja akamilishe jukumu lake la kila siku.
“Tulipopewa miradi iliyo nje ya majukumu yetu, tuliona tusingefanikiwa kwa kuwa watu wetu wamebobea katika mambo mengine, lakini Mhandisi Mfugale alikuwa akitutoa wasiwasi na kutupa mbinu za utekelezaji,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (ERB), Profesa Ninatubu Lema, amesema Mhandisi Mfugale amekuza wahandisi vijana 306 hadi sasa.
Amesema kwa mara ya mwisho aliwatembelea wanafunzi wa Uhandisi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo aliwafundisha kujishusha na kufanya kazi kwa weledi na umakini.
Erasto Mfugale ni mdogo wa Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kiongozi huyo ndiye aliyeachiwa majukumu ya kusimamia familia tangu baba yao alipofariki mwaka 2002.
Amesema Juni 27 alikuwa naye nyumbani kwake Temboni jijini Dar es Salaam kwa kikao maalumu na alimwambia kuwa kesho yake atakuwa na safari ya kwenda Dodoma kwa shughuli za kikazi.
Amebainisha kabla ya kufariki Mhandisi Mfugale asubuhi alipata chai nyumbaji kwake Dodoma, kisha alikwenda kazini ndipo baadaye walipopigiwa simu kupewa taarifa ya msiba.
Akitoa ushuhuda wa marehemu, Aron Mfugale, ambaye ni mtoto wa Mhandisi Mfugale, amesema baba yao aliwafunzisha kuwa na imani ya kumcha Mungu, kutojikweza kwa nafasi ya baba yao na kutoa msaada kwa wenye uhitaji.
Amefafanua kuwa Mhandisi Mfugale alipenda ukweli, kwani hata alipokosewa akiambiwa ukweli husamehe.
“Alikuwa akitusisitiza kwa kutuambia kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza akiwa na maana kwamba yeyote kati yetu atakayeishi kwa kutumia umaarufu na jina lake, imekula kwake,” amesema.
Ibada ya kumuaga Mhandisi Mfugale iliongozwa na Paloko Msaidizi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dennis Wigila.
Mbali na Rais Samia hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wengine mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mama Mary Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Said.
Mhandisi Mfugale alifariki Juni 29, mwaka huu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, ameacha mjane na watoto wanne.
Tangu mwaka 1977 aliajiriwa kutumikia Wizara ya Ujenzi na aliendelea kwa kuhama nafasi mbalimbali ndani ya Wizara hiyo hadi anafariki akiwa ameitumikia kwa miaka 41.
Mhandisi Mfugale amefariki akiwa na umri wa miaka 68, alizaliwa Disemba mosi mwaka 1953, Ifunda mkoani Iringa.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kwenda mkoani Iringa kesho jioni kwa ajili ya maziko yatakayofanyika jumatatu.
Na JUMA ISSIHAKA



























