Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy atafikishwa mahakamani mnamo mwaka 2025 kujibu tuhuma za rushwa na ufadhili haramu alioshirikiana na anayedaiwa kuwa raia wa Libya aliyefanikisha mpango wa Rais huyo kuwania urais mwaka 2007. (ofisi ya mwendesha mashtaka ya kifedha ilisema Ijumaa.)
Sarkozy, ambaye ni mtu muhimu katika siasa za Ufaransa ingawa hana tena wadhifa wowote wa kuchaguliwa, amekuwa akikanusha shutuma hizo. “Hakuna uthibitisho hata mdogo unaonihusisha mimi na matukio ya namna hiyo,” alisema katika mahojiano mwaka 2018.
Rais huyo wa zamani wa kihafidhina, alikuwa madarakani kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2012, anaweza kupewa adhabu ya kifungo cha mpaka miaka 10 jela endapo atakutwa na hatia katika kesi hiyo. Sarkozy pia anapambana na kesi nyingine mbalimbali za kisheria.
Katika kesi hii, atasimama mahakamani kwa tuhuma za “kuficha ubadhirifu wa fedha za umma, rushwa, ufadhili haramu wa kampeni na njama za kihalifu kwa nia ya kutenda uhalifu ambao adhabu yake ni kifungo cha miaka 10 jela,” ilisema ofisi ya mwendesha mashataka.
Miongoni mwa watu wengine 12 wanaokabiliwa na kesi hiyo ya Sarkozy ni aliyekuwa mtu wake wa karibu Claude Gueant na kiongozi wa ufadhili wa kampeni wa wakati huo Eric Woerth pamoja na aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani Brice Hortefeux.
Usikilizaji wa awali umepangwa kufanyika Machi 7, 2024, ofisi ya mwendesha mashtaka ilisema, wakati kesi yenyewe imepangwa kufanyika kati ya Januari 6, na Aprili 10 mwaka 2025.
Sarkozy mwenye umri wa miaka 68, alishindwa katika rufaa mwezi Mei dhidi ya hukumu ya tuhuma za rushwa na ufisadi iliyotolewa mwaka 2021. Timu yake ya wanasheria iliahidi kupinga hilo katika mahakama ya juu ya Ufaransa.
Rais aliyemtangulia Sarkozy wa kihafidhina, Jacques Chirac alipatikana na hatia ya rushwa mwaka 2011, miaka minne baada ya kuondoka madarakani.
Chanzao cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.