RAIS wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, amesema kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini humo, masharti ya kupambana na maambukizi hayo yataendelea kutekelezwa hadi mwisho wa Julai, mwaka huu.
Miongoni mwa masharti hayo ni kuendelea kufungwa kwa shule na maeneo ya kuuzia vileo, lakini pia watu hawaruhusiwi kutembea nje kati ya saa tatu usiku mpaka saa 10 Alfajiri.
Imeelezwa kuwa nchini humo, wimbi la tatu la janga la corona kwa kirusi kipya aina ya Delta, linasambaa kwa kasi kubwa ikilinganishwa na wimbi la kwanza na la pili.
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), limetoa taarifa hiyo jana, ambapo kitakwimu limeonesha kuwa idadi ya waathirika inaongezeka mara mbili zaidi kila baada ya wiki 6.
Limesema kirusi hicho kipya cha Delta kinasambaa haraka katika baadhi ya nchi na tayari kimeripotiwa katika nchi 16, kati ya hizo 9 kinasambaa kwa kasi zaidi.
Taarifa zinasema raia wa nchi hiyo, wanaendelea kuwa wakaidi dhidi ya maagizo ya serikali kuhusu mapambano ya virusi hivyo.
JOHANNESBURG, Afrika Kusini