Na HANIFA RAMADHANI NA EMMANUEL MOHAMMED, ZANZIBAR
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib, ametoa onyo kwa wananchi wanaokwenda kuchukua mchanga katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Amesema kuna baadhi ya watu wanaokwenda kumuombea dua marehemu huyo kaburini kwake na baadae wamekuwa wakichota mchanga katika kaburi hilo na kuondoka nao kwa madai ya kuwa unanukia harufu ya miski, kitendo ambacho hakikubaliki.
Mkuu huyo wa mkoa, aliyasema hayo jana, alipotembelea eneo la kaburi la Maalim Seif, baada ya kupata malalamiko hayo kutoka kwa ndugu wa karibu wa familia hiyo.
Aliiomba familia hiyo iendelee kuwazuia watu wanaokwenda kaburini hapo kwa lengo la kuchukua mchanga huo, kwa sababu haifahamiki sababu za watu kufanya hivyo na haijulikani wanakwenda kuufanyia nini.
“Nikiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, naomba nilitolee tamko jambo hili, watu waje kama wanavyokuja kuomba, dua lakini wasichukue mchanga,” alisema.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Juma Said Khamis, alisema watu wanaokwenda kumuombea dua Maalim Seif na baadae kuchukua mchanga, siyo jambo zuri kwa sababu ni katika mambo ambayo hayapendezi.
Alisema watu kuruhusiwa kusoma dua ni jambo la kawaida, lakini mtu akichukua mchanga, atakuwa anakosea na kwamba, kwa yeyote ambaye atafanya jambo hilo, atakuwa amekosea na sheria itachukua mkondo wake.
Kwa upande wake, Kiongozi wa familia ya Maalim Seif, Seif Ali Seif, alisema watu huja katika kaburi la kiongozi huyo na kuchukua mchanga kwa madai ya kwamba una harufu nzuri.
“Wengine wanasema mchanga huo unanukia mafuta mazuri, wengine wanasema unanukia harufu ya miski, mimui huwaambia waunuse na baadae wauache hapo hapo, wasiuchukue na kwenda kuufanyia mambo ya kishirikina,” alisema.
Kiongozi wa dini wa mkoa huo, Sheikh Omar Hamid, alisema inajulikana kwamba, Maalim Seif, anapendwa sana, lakini kitendo cha kuchukua mchanga siyo kizuri kwa sababu wengine huchukua kwa nia mbaya.
“Najua kama tunampenda sana kiongozi wetu huyu, lakini nisema tu mahaba haya yatasababisha kukufuru, hivyo niombe tu huu mchanga tuuache na tuendelee kumuombea dua mwenzetu huyu,” alisema.