MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka, amezuia kupitishwa kwa fedha sh. milioni 46 zilizopangwa kutumika kutoa mafunzo kwa maofisa watendaji wa wilaya ya Dodoma Mjini, yaliyopangwa kufanyika mkoani Mbeya.
Akizungumza katika mkutano na maofisa watendaji wa wilaya ya Dodoma Mjini, Mtaka alisema serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, aliwataka viongozi wote wa mkoa, kutotoka katika maeneo yao ya kazi kwa kisingizio cha kufanya ziara hadi kupata kibali maalumu kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango au Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema hatoweza kuidhinisha fedha hizo ziende kutumika katika mafunzo kutokana na ubabaishaji wa baadhi ya viongozi kutaka kuchukulia kama fursa ya kufanya ubadhirifu wa fedha hizo, kwani hazina maelezo ya kuridhisha.
“Jambo la kushangaza, juzi Waziri Ummy katangaza viongozi hakuna kusafiri kwenda popote ili kutekeleza majukumu yao hususan kwa fedha hizi zilizotengwa kila mkoa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Tunataka kuona watu wanawajibika katika nafasi zao za kazi mambo ya kuidhinisha fedha kama hizi kwa suala la semina, tunadhoofisha utendaji kwa watumishi. “Lazima ifikie mahali, mkurugenzi unazuia matumizi ya fedha yasiyo na uhitaji,” alisema.
Aidha, Mtaka aliwataka watendaji kushughulikia kero za wananchi, si kuwaacha hadi kufika katika ngazi ya mkoa na kuleta sintofahamu kwa baadhi ya viongozi wa juu kuhusu utendaji wao.
Alisema wananchi wamekuwa wakilalamika kutofanyiwa kazi malalamiko yao pindi wakileta katika ofisi za kata, matokeo yake, wamekuwa wakikimbilia ofisi za mkoa bila kufuata utaratibu na kuonyesha taswira mbaya kwa watendaji.
“Jukumu langu ni kushughulika na matatizo ya mkoa wenye wilaya tano.
“Nashangaa naletewa kesi ambazo nyingine zinatakiwa kuishia katika ofisi zenu au kuzipeleka kwa mkuu wa wilaya. Sitaki kuona zinakuja moja kwa moja ofisi ya mkoa, viongozi wengine wanafanyaje wajibu wao,” alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwatano, Selemani Mubarack, alisema wamekuwa wakipeleka malalamiko ya wananchi katika ofisi za mkuu wa wilaya na kushindwa kufanyiwa kazi haraka, hivyo kusababisha baadhi ya wananchi kushindwa kuwaamini.
Na Benedict Mwasapi, Dodoma





























