MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Binilith Mahenge, amewahimiza viongozi wa serikali, vyama vya siasa na madhehebu ya dini kushirikiana ili watu wenye miaka 18 na kuendelea, wanapata chanjo ya Uviko 19.
Dk. Mahenge aliyasema hayo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa (PHC), kilichofanyika ofisini kwake.
Alisema kazi ya utoaji chanjo dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19 mkoani Singida, halikufanyika kwa kiwango kilichokusudiwa.
“Ili tuweze kufikia malengo lazima tushirikiane sote. Uhamasishaji tuupe kipaumbele, tutembelee nyumba kwa nyumba. Chanjo hii dhidi ya Corona ni muhimu mno.
“Kuna nchi za wenzetu wanawavutia watu wao wachanje kwa kutoa zawadi. Zipo nchi hawaruhusu watu wasiochanjwa kuingia hotelini au madukani.
“Kwa ujumla tunahitaji watu wenye afya bora au uhakika, hivyo waone umuhimu wa kuchanjwa,” alisema.
Alieleza kuna umuhimu katika nyumba za ibada za madhehebu ya dini, kukawa na mahema au maturubai kwa ajili ya waumini kupata chanjo ya corona.
Aidha, alisema chanjo ndiyo njia pekee yenye ufanisi katika kukinga na kudhibiti kusambaa kwa Uviko-19.
“Chanjo ya corona inawezesha kinga mwilini kupambana na virusi vya Uviko-19 pale mtu anapoambukizwa. Inatolewa bure, inapatikana nchi nzima katika hospitali na vituo maalumu,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Alhaj Issa Nasoro, alisema chanjo ya corona ina faida nyingi ambazo, mojawapo ikiwa kuwawezesha waumini kushiriki ibada ya hija.
Pia, alisema kutokana na umuhimu wa chanjo ya corona, wamekuwa wakitumia mihadhara kuhimiza waumini kupata chanjo hiyo kwa faida yao na watu wengine.
Na NATHANIEL LIMU, SINGIDA



























