WATUMISHI wa Umma 63 wakiwemo Wakurugenzi na Wakuu wa Idara, wamechukuliwa hatua kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya kupeleka asilimia 40 ya mapato katika shughuli za maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festo Dugange, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi (CCM), George Mwenisongole.
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua mpango wa serikali wa kuziwajibisha halmashauri ambazo zinajiweza kimapato, lakini hazipeleki asilimia 40 ya mapato ya ndani katika shughuli za maendeleo kama zinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, badala yake zimekuwa zikiwalazimisha wananchi wachangie.
Akijibu swali hilo, Dk. Dugange alisema mwongozo wa uandaaji wa bajeti unaotolewa kila mwaka na serikali, unatoa maelekezo kwa halmashauri zote nchini kutenga sehemu ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema halmashauri zenye mapato yasiyolindwa chini ya sh. bilioni tano, zinapaswa kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani na halmashauri zenye mapato yasiyolindwa zaidi ya sh. bilioni tano zinapaswa kutenga asilimia 60 ya mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Katika mwaka wa fedha 2019/2020, kiasi cha fedha sh. bilioni 216.4 kimetumika kwa shughuli za maendeleo sawa na asilimia 70.87 ya fedha zilizopaswa kutumika katika miradi ya maendeleo,” alisema.
Alifafanua kuwa, katika mwaka wa fedha 2020/2021, kiasi cha sh. bilioni 279.7 kimetumika katika miradi ya maendeleo sawa na asilimia 92 ya fedha zilizopaswa kupelekwa katika miradi ya maendeleo.
Naibu waziri huyo, alieleza kuwa, serikali imeshawachukulia hatua watumishi 63, wakiwemo wakurugenzi na wakuu wa idara kwa kushindwa kutekeleza maagizo hayo na utaratibu huo ni endelevu.
“Napenda kutoa rai kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuhakikisha maelekezo haya yanatekelezwa kwa ufanisi,” alisema.





























