ALIPOONDOKA Ubelgiji, hakuwa na uhakika kama atarudi tena katika nchi hiyo ambayo ilimpa umaarufu zaidi na kupata ofa mbalimbali katika Ligi ya Uingereza. Huyu si mwingine ni Mbwana Ally Samatta, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Samatta alicheza kwa mafanikio makubwa nchini Ubelgiji baada ya kusajiliwa na timu ya KRC Genk na kung’ara kwa misimu mitano. Nyota ya Genk ilimpa Samatta ulaji na kulamba dili la kujiunga na Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza alikotua msimu wa 2020-2021.
Hata hivyo, hakudumu Aston Villa kwani alipelekwa kwa mkopo Fenerbahce inayoshiriki Ligi ya Uturuki.
Kuondoka kwake Uingereza, kulionekana kufi fi sha nyota ya mshambuliaji huyo hatari ambaye safari yake ya kucheza soka la kimataifa ilianzia TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Akiwa anajiandaa na msimu mpya katika kikosi cha Fenerbahce, inaelezwa kuwa Samatta hakuwa na uhakika wa kucheza katika kikosi cha kwanza. Sababu ya nyota huyo ya kutokuwa na uhakika wa kupata namba ni baada ya Fenerbahce kumsajili mshambuliaji Mesut Ozil kutokea Arsenal, ilibidi amwachie jezi namba 10 na kubadilishiwa na kupewa namba 15.
Hata hivyo, waswahili wanasema ‘Bahati ya Mtu Usiilalie Mlango Wazi’, kwani wiki iliyopita, ndoto ya Samatta kurudi Ubelgiji ilitimia baada ya kusajiliwa kwa mkopo katika kikosi cha Royal Antwerp, akitokea Fenerbahce kwa mkataba wa miaka mitatu.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, amesajiliwa kwa dau la Euro milioni nne (zaidi ya sh. bilioni 10 za Tanzania). Usajili wa nyota huyo ulimuibua baba yake, Ally Samatta, aliyetoa siri na kusema mwanawe alitamani sana kurudi Ubelgiji na ndoto yake imetimia.
Ally alisema, muda mfupi baada ya mwanawe kutia saini kujiunga na klabu hiyo, alizungumza naye na kumuelezea furaha yake na kiu ya kurejea tena Ubelgiji. “Alikwenda kucheza Uturuki lakini akili yake yote ilikuwa Ubelgiji, kuna wakati nilizungumza naye na kumhoji ni wapi zaidi alitamani apate muda mwingi wa kucheza soka”.
“Aliniambia bado kuna kitu hajamaliza kufanya Ubelgiji, huko ndipo kutakapompa mafanikio zaidi ya kucheza tena Ligi Kuu ya Uingereza,” alisema Ally.
Aliongeza kuwa, Samatta amefanya uamuzi sahihi na amefurahi kumuona akicheza katika Ligi ya Ubelgiji msimu huu. Anasema ana matumaini atang’ara kwa kuwa ana uzoefu na ligi ya nchi hiyo ambayo hajacheza msimu mmoja.
“Kuna wakati nilipata hofu ya kiwango chake baada ya kujiunga na Fenerbahce akitokea Aston Villa, lakini baadae niliona jinsi wenzake wanavyocheza, walikuwa wakitumia ubabe, naamini kiwango chake kitarudi kama zamani,” aliongeza.
Baba huyo anasema aliwahi kumwambia mwanawe kuwa ni lazima aondoke Uturuki na kutafuta timu nyingine na ndio maana aliposikia habari ya kurudi tena Ubelgiji alifurahi.
Wakati Ally akielezea undani wa usajili huo, kaka wa Samatta, Mukhsin alisema ana matumaini ndugu yake atawika kwa kuwa anarejea katika ligi anayoifahamu vyema.
Anasema anatambua juhudi za Samatta na ana imani ataanza kuonyesha makali kwa kuleta ushindani dhidi ya wachezaji wenzake kwani alishacheza kwa mafanikio katika Ligi Kuu ya Ubelgiji.
“Ninatambua juhudi aliyonayo Samatta, nina imani ataanza kufanya vizuri katika timu yake mpya na kuhakikisha anaipatia mafanikio makubwa kuanzia msimu huu. “Awali alishacheza katika Ligi hiyo, hivyo sio sehemu ngeni kwake, nina matumaini makubwa atang’ara na kuendelea kutengeneza rekodi katika mchezo wa soka,” anasema.
KAULI YA MCHAMBUZI
Mchambuzi Ally Mayay, anasema Samatta hakuwa na nafasi ya kucheza kwa kiwango bora Uturuki, hivyo amefanya uamuzi mzuri wa kuondoka na kurejea Ubelgiji.
“Ni maamuzi mazuri aliyofanya kutokana na utashi wake, hivyo ninampongeza na nina imani atapata nafasi kubwa ya kucheza na kuonyesha uwezo wake,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Yanga.
AHADI
Gazeti hili lilipomhoji Samatta juu ya maisha mengine mapya ya Ubelgiji, alisema amefurahi kurudi nchini humo ambapo bado alikuwa akihitaji kutumika.
“Hii ni safari nzuri sana kwangu, kutoka Uturuki kurudi Ubelgiji ni nafasi ya kwenda kurudisha makali yangu, ligi ya nchi hiyo ilinipenda na mimi niliipenda,” alisema.
Samatta alisema ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika ligi hiyo ambayo ndiyo iliyompa mafanikio.
Aliongeza kuwa, huu ni wakati wa kufanya mazoezi kwa bidii na kuendelea kuitangaza Tanzania katika ramani ya soka.
SAFARI KIMATAIFA
Samatta alijiunga na Simba akitokea African Lyon mwaka 2010 ambapo alicheza hadi 2011 kabla ya kujiunga na TP Mazembe ya DR Congo alipocheza hadi mwaka 2016.
Alisajiliwa Fenerbahce akitokea Aston Villa ya Uingereza alikotua msimu wa mwaka 2020-2021, akitokea KRC Genk ya Ubelgiji alikong’ara kwa misimu mitano mfululizo akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Katika misimu yake mitano KRC Genk, Samatta aliichezea mechi 191 akiifunga mabao 75 katika Ligi Kuu ya Ubelgiji na michuano ya kimataifa.
Baadaye alitimkia Genk alipocheza hadi mwaka 2020 kabla ya kutua Aston Villa na baadaye kwenda kwa mkopo Fenerbahce.
Antwerp ipo katika nafasi ya 15 katika Ligi Kuu ya Ubelgiji, ikiwa na pointi tano, baada ya kucheza mechi tano msimu huu.
Na VICTOR MKUMBO