Na Mwandishi Wetu
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania naIndia, zimekubaliana kukuza ushirikiano wa kihistoria
kati ya nchi mbili hizo hadi kuwa ushirikiano wa ngazi ya kimkakati. Katika ziara yake ya kitaifa ya siku tatu nchini humo, Rais Dk. Samia ameihakikishia India kwamba Serikali itaimairisha urafiki na ushirikiano uliopo uliodumu
kwa miongo kadhaa.
Alisema mazungumzo ya ‘uwazi na amani’ na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa India, Narendra
Modi, yameainisha shauku ya pande mbili hizo kujitolea kuimarisha na kukuza ushirikiano uliopo
katika hatua ya juu zaidi.
“Tumekubaliana kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano na pia kukuza ushirikiano wetu hadi hatua ya Mfumo wa Ushirikiano wa Kimkakati,” Rais Samia alisema hayo katika mkutano wao wa pamoja na wanahabari uliofanyika jijini New Delhi jana.
Akiielezea India kama ndugu, Rais Samia alisema ameridhishwa na kukua kwa biashara na uwekezaji
kati ya nchi hizo mbili umekuwa katika njia nzuri ya maendeleo.
“Hadi mwaka 2022, biashara kati ya nchi mbili hizo ilikuwa ya thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.1,
hatua ambayo imeifanya India kuwa mshirika wa tatu kwa biashara na nchi ya tano kwa uwekezaji mkubwa
Tanzania,” alisema.
Rais alipokea ombi la India kufungua tawi la Taasisi ya Teknolojia India (IIT) nchini. Tanzania na India zimekuwa zikishirikiana katika nyanja nyingi kama vile maji safi na salama, ulinzi na usalama.