* Ni miongoni mwa wanawake 100 wenye uwezo mkubwa duniani
* Yatambua uwezo wa Samia kwa mwaka wa pili mfululizo
* Awekwa kundi moja na wanawake wenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani
***
RAIS Samia Suluhu Hassan ametajwa na jarida la Forbes kwa mwaka wa pili mfululizo kuwa miongoni mwa wanawake 100 wenye ushawishi, nguvu na uwezo mkubwa wa uongozi duniani katika orodha ya mwaka 2022.
Rais Samia ametambuliwa katika orodha hiyo ambayo pia amejumuishwa na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, Rais wa Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya, Christine Lagarde na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Kristalina Georgieva, na aliyekuwa mke wa mmoja wa watu matajiri zaidi duniani Jeff Bezos, Mackenzie Scott. nao pia wametambuliwa kwenye orodha hiyo inayoheshimiwa duniani.
Leyen ameshika nafasi ya kwanza katika orodha hiyo ya mwaka huu, wakati Samia yuko nafasi ya 95.
Kwa upande wake, Rais Samia ambaye mwaka jana alishika nafasi ya 94 kwenye orodha hiyo ya Forbes ya wanawake wenye nguvu zaidi duniani, amejipatia sifa kutokana na uongozi wake shupavu kwenye kukabiliana na janga la corona nchini Tanzania tangu aingie madarakani Machi 2021.
Sifa moja kubwa ambayo watu waliowahi kufanya kazi na Rais Samia kwa karibu wanaisema na ambayo si watu wengi wa nje wanaifahamu ni uwezo wake mkubwa wa kiuongozi.
Benki ya Dunia hivi karibuni iliipongeza serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia kwa “miujiza ya kiuchumi” kutokana na kuweza kudhibiti mfumuko wa bei wakati nchi nyingi duniani zinakabiliwa na janga la uchumi kutokana na vita ya Ukraine.
Rais Samia ameelezwa na wachambuzi wa siasa na uongozi nchini na wa kimataifa kuwa huenda akaweza historia ya kuwa mmoja wa viongozi mahiri siyo barani Afrika tu, bali duniani kote.
Tangu aingie madarakani, Rais Samia ameongeza uwekezaji wa serikali kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu na amewekeza pesa nyingi kwenye sekta za maji, elimu na afya.
Katika nyanja ya elimu, alipoingia madarakani, serikali ilikua inatoa elimu bure hadi kidato cha nne, lakini akaongeza elimu bure hadi kidato cha sita.
Rais Samia pia ameonesha umahiri wa uongozi kwa kuongeza makusanyo ya kodi na kuifanya Tanzania ing’are kwenye nyanja ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa.
Samia amepongezwa pia kwa kuleta utulivu wa kisiasa nchini na kwa kuagiza serikali yake ianze mchakato wa kuleta mageuzi ya haki za jinai.
Rais Samia ameanzisha mazungumzo na viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na kuunda kikosi kazi ambacho, pamoja na mambo mengine, kimependekeza mageuzi makubwa ya sheria za uchaguzi nchini na kukamilishwa kwa mchakato wa katiba mpya.
Samia pia amerejesha imani ya wafanyabiashara na wawekezaji wa nje na ndani kwa Tanzania, ikiwemo kufanya mazungumzo na tajiri mkubwa zaidi Afrika, Aliko Dangote, na kuanzisha majadiliano na makampuni makubwa ya nishati duniani ambayo yanapanga kuwekeza zaidi ya Shilingi trilioni 90 kujenga kiwanda cha kuchakata gesi asilia (LNG) nchini.