TIMU ya Taifa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’, imefuzu Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cameroon.
Serengeti Girls ilipata ushindi huo katika mchezo wa pili wa raundi ya nne kufuzu fainali hizo uliochezwa katika dimba la Amaan, Zanzibar, ikiwa ni wiki mbili tangu iliposhinda mabao 4-1, katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Yaounde, Cameroon.
Bao pekee lililofungwa kwa kichwa dakika ya 48 na Neema Paul akiunganisha kona iliyochongwa kutoka upande wa kulia, limeipeleka Tanzania katika fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 30, mwaka huu nchini India.
Timu zilianza mchezo kwa kushambuliana kwa zamu huku kukiwa na piga nikupige ndani ya dakika 15 za mwanzo.
Dakika ya 20, Aisha Juma alipata nafasi ya kufunga lakini mpira aliopiga ulipaa juu na kutoka nje.
Dakika ya 25, Clara Luvanga alikuwa katika nafasi ya kufunga, lakini shuti hafifu alilopiga lilipaa juu ya goli na kutoka nje.
Cameroon nayo ilipata nafasi katika dakika ya 28, 33, 40 na 41 lakini mashuti yaliyoelekezwa langoni mwa Serengeti Girls yalidakwa na kipa Husna Mtunda.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu kwenda mapumziko bila kufungana na kipindi cha pili kilianza kwa Tanzania kufanya mashambulizi makali yaliyozaa bao.
Hata hivyo, kipindi cha pili kilikuwa cha kuvuta nikuvute kwa timu zote kutafuta ushindi wa aina yeyote ile, lakini hadi dakika 90 zinakamilika Serengeti Girls ilitoka uwanjani kwa shangwe la kufuzu Kombe la Dunia.
Baada ya mechi, mashabiki walilipuka kwa furaha na kupiga kelele za kuipongeza Serengeti Girls huku wakiimba “Tunaenda Kombe la Dunia, Mama Samia tumekupa furaha” na wachezaji wakiangua vilio vya furaha na kukumbatiana kama ishara ya kupongezana.
Kikosi hicho kilichoondoka Zanzibar jana usiku, leo kinakwenda Bungeni jijini Dodoma kwa ajili ya kupongezwa baada ya kuipeperusha vyema bendera ya nchi.
Tanzania: Husna Mtunda, Noela Patrick, Joyce Lema, Clara Luvanda, Aisha Juma, Zainab Ally, Diana Mnally, Neema Kinega, Christer Bahera na Veronica Mapunda.
Cameroon: Cathy Biya, Marlene Essimi, Mana Lamine, Oceane Nana, Achta Toko, Camila Daha, Bernadette Mbele, Elvin Linho, Angela Megueyepagueyep, Melanie Keumodjo.
Na SOPHIA ASHERY, Zanzibar