Serikali imepongeza taasisi na watu binafsi kwa kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu yakiwemo majengo ya kisasa mkoani Dodoma na kuufanya mji huo mkuu kukua kwa kasi zaidi.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa duka kubwa la kisasa la kuuza rangi mkoani Dodoma zikiwemo za kupaka kwenye nyumba, Mtendaji Mkuu wa Insignia Limited, watengenezaji wa rangi za Coral Paints, Mike Fischer amesema kupitia sekta ya ujenzi, wameamua kuwekeza mkoani humo, ili kuiunga mkono Serikali katika ukuaji wa haraka wa mji huo mkuu.
“Ukuaji wa majiji mengi duniani unatokana na ujenzi wa miundombinu bora na yakisasa ambayo inapendezesha majiji hayo na kuvutia uwekezaji,”
“Toka Serikali ihamie Dodoma, tumeshuhudia ukuaji wa kasi wa mji huu kutokana na ujenzi wa miundombinu yakiwemo majengo ya kisasa ya Serikali na taasisi zake za umma, ofisi za mashirika ya ndani na ya kimataifa na ujenzi wa nyumba bora za wananchi,”
“Hivyo tumeona ni vema na sisi tukawa ni sehemu ya historia ya mapinduzi haya ya mkoa huu kupitia sekta ya ujenzi na uwekezaji kwa kufanya kazi pamoja na wakandarasi na wadau wengine muhimu wakiwemo mafundi,”
“Hivyo tumeamua kuwekeza Dodoma ili kuendelea kuufanya mji huu kuwa mzuri zaidi na wenye kupendeza kwa kuwasogezea huduma zaidi wananchi, Serikali na taasisi kutumia bidhaa zetu bora na za bei nafuu, ili kuendelea kuujenga mji wetu na kuufanya moja ya majiji mazuri duniani”, amesema.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mauzo na Biashara Navdish Sharma amesema sekta ya ujenzi mkoani Dodoma imepata mbia wa kushirikiana naye kwa kupeleka karibu mahitaji yote ya rangi nzuri zinazotengenezwa kwa ubora wa hali ya juu hapa nchini.
“Watumie vizuri uwekezaji mkubwa tulioufanya hapa Dodoma, ili kukuza zaidi sekta ya ujenzi na kuleta matokeo chanya,”amesema.
Adam Kefa, Mkuu wa Kitengo cha Masoko amesema wana mipango ya kufungua maduka mengine makubwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini, ili kupeleka huduma bora kwa wananchi, ambao ni wabia wakubwa wa bidhaa zinazotengenezwa na kampuni hiyo.
Na ndio maana amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa na utaratibu wa kurudisha kwa jamii kwa kutoa misaada kila inapowezekana, ambapo imekuwa na utaratibu kutoa misaada kama sehemu ya kurudisha kwa jamii.
“Jamii ya Watanzania ni sehemu ya kampuni yetu,”
“Ndio maana tumekuwa mstari wa mbele pia katika ukarabati wa miundombinu kama vile shule na vituo vya watoto wenye uhitaji katika sehemu mbalimbali ikiwemo Dodoma na Dar es Salaam,”amesema