NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe, amesema serikali inatarajia kutumia sh. bilioni 100 kujenga miundombinu ya Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius Nyerere, Butiama mkoani Mara.
Profesa Mdoe ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya Waandishi wa Habari iliyoandaliwa na Wizara hiyo, ikilenga maboresho na matumizi ya fedha zilizotolewa na serikali kukarabati na kununua miundombinu ya kisasa ya kujifunzia na kufundishia.
Profesa Mdoe amebainisha kuwa kukosekana kwa usajili wa kudumu kwa chuo hicho kunatokana na kutokamilika kwa miundombinu.
“Chuo ni kikubwa kipo Butiama lakini sasa tunataka kukijenga na kukipatia usajili ili kikamilike,” amesema.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo, amefafanua maombi ya mkopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, yataanza kuchakatwa utakapofika ukomo wa muda uliopangwa.
Amewasisitiza wanafunzi kufuata maelekezo na kuhakikisha wanajaza fomu kwa usahihi huku akionya kutopeleka fomu kabla ya kukamilisha usajili na kwamba dirisha hilo litafungwa Agost 31, mwaka huu.
Naibu Katibu Mkuu ameongeza kuwa serikali imeongeza fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu hadi kufikia sh. bilioni 570 na matarajio ni kuwanufaisha wanafunzi 160,000, huku kwa mwaka wa kwanza pekee wakitarajiwa kukopeshwa 620000.
Na Happiness Mtweve, Iringa



























