SERIKALI imesema ina mkakati wa kupunguza gharama za kusafisha figo nchini ikiwemo kununua vifaa tiba na vitenganishi moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji.
Kauli hiyo ilitolewa Bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mariam Kisangi.
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wagonjwa wa figo kupata matibabu ya kusafishwa figo kwa gharama nafuu.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Dk. Mollel alisema katika kukabiliana na hali hiyo, Mswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote utakapokamilika utakuwa suluhisho la kudumu la matibabu ya ugonjwa huo.
“Hata hivyo, Sera ya Afya nchini inaelekeza hakuna Mtanzania anayepaswa kufariki dunia kwa sababu ya kukosa fedha, hivyo serikali imekuwa ikitoa msamaha wa matibabu kwa wasio na uwezo ambao wametimiza vigezo,” amesema.