Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imekubali ombi la Klabu ya Yanga kugharamia safari ya mashabiki kwenda nchini Afrika Kusini kuisapoti timu yao wakati wa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Hayo yamesemwa leo na Rais wa Klabu ya Yanga, Eng. Hersi Said wakati akizungumza kwenye mkutano na wanahabari pamoja na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamisi Mwinjuma maarufu kama Mwana FA.
“Tunafahamu Klabu yetu ya Young Africans SC ina mchezo mwingine wa pili kule Afrika Kusini hivyo Uongozi wenu umefanya jitihada za kupeleka Ombi katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Waziri wetu Mhe. Dk. Damas Ndumbaro la kusafirisha mashabiki kwa njia ya Basi na tunaishukuru Wizara kwa kukubali Ombi letu.
“Wizara itahudumia gharama zote za safari ya kuelekea Afrika kusini yenye Wanachama na Mashabiki wetu 48 kuanzia Nauli mpaka pesa ya kujikimu, hivyo sisi Young Africans tunaishukuru sana Wizara.
“Hapo mwanzo tulitangaza watu watakaosafiri walipaswa kuwa na shilingi laki 6 na tulipata watu 30, niwahakikishie baada ya Wizara kukubali kusafirisha Wanachama na Mashabiki wetu,zile laki 6 zitarudishwa kwa wenyewe.
“Niwatakie safari njema na nina imani safari yetu ya kurudi itakuwa nzuri kwakuwa tutarudi tukiwa tayari tumeshafuzu hatua ya nusu Fainali” Rais wa Young Africans SC Eng. Hersi Said akiongea na Wanahabari wakati wa kuwaaga Wanachama na Mashabiki wanaosafiri kuelekea Afrika Kusini Makao Makuu ya Klabu Jangwani,” amesema Hersi.