SERIKALI imesema itahakikisha inaboresha ushirikiano na mataifa ya nje katika utendaji kazi kuhusu suala zima la ulinzi na usalama ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa kimtandao.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Jimmy Yonazi, ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya siku tano kwa wapelelezi pamoja na maaskari wa chumba cha mashtaka wa Tanzania na Zanzibar lengo likiwa ni kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya uhalifu wa Mtandao.
Dk. Yonazi amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa ajili yakujenga uwezo wa Nchi hivyo jukumu lao ni kuhakikisha wanalinda usalama wa Nchi.
“Kama Serikali tutaendelea kufanyia kazi ya mashirikiano baina ya nchi yetu na nchi nyingine katika kuhakikisha tunaimarisha masuala ya mawasiliano ya TEAHAMA ili kukabiliana na uhalifu wa kimtandao,” alisema
Pamoja na mambo mengine amesema uhalifu wa kimtandao ni mpana na kila siku teknolojia inakuwa hivyo ni muhimu kuhakikisha kila mara wanajengeana uwezo ili kwenda na ulimwengu wa kidijitali.
Amebainisha kuwa, Serikali imechukua hatua kwa kutunga Sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 ili kuweza kukabiliana na masuala ya uhalifu wa kimtandao ambao umekuwa ukishika kasi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, DCI Camilius Wambura, amesema Mafunzo hayo yataleta matokeo chanya kutokana na mbinu walizopata ili kukabiliana na uhalifu wa kimtndao kwani mataifa yatawasaidia katika kubadilishana taarifa.
Wambura amewataka wapelelzi hao pamoja na askari kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu na nidhamu katika utendaji kazi wao kwani tabia za wachache zimekuwa zikiharibu taswira ya Jeshi jambo ambalo si jema.
Pia amewataka kufanya kazi kwakushirikiana ili kuweza kufikia malengo.
Na Happiness Mtweve, Dodoma





























