SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua mwongozo wa matibabu, ambao umewezesha kuwepo na ongezeko la dawa mpya 101 katika orodha ya dawa muhimu zikiwemo za upasuaji, shinikizo la damu na kisukari ili imarisha huduma za afya nchini.
Pia kupitia mwongozo huo serikali imezingatia matibabu ya ugonjwa wa homa ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (covid-19).
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.Dorothy Gwajima, alipokuwa akizindua mwongozo huo ambao umeandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikisha wadau mbalimbali ikiwamo Vyama vya kitaaluma na wadau wa maendeleo.
Dk. Gwajima amesema mwongozo huo umepitiwa kukidhi maboresho ya huduma za matibabu katika ngazi ya afya ya msingi, au kukidhi kupanuka kwa huduma za kibingwa na kutoa mwongozo wa kutibu magonjwa mapya yanayoibuka
Pia amesema katika toleo hilo la sita la mwongozo huo, ni pamoja na kutoa mwongozo juu ya menejimenti na matibabu ya ugonjwa mpya wa corona, ambayo yametolewa ufafanuzi katika sura ya magonjwa ya mlipuko.
“Mwongozo huo umepitiwa ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kitabibu na mabadiliko ambayo yameanishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na mashirika mengine ya kitaifa na kimataifa kulingana na tafiti mbalimbali,” amesema.
Waziri huyo amezungumzia orodha mpya ya dawa 101 zilizoongezwa, kuwa baadhi ya dawa zimeongezwa ili kukidhi maboresho ya huduma za kibingwa katika kupandikiza figo.
Pia amefafanua kuwa katika kuimarisha huduma za afya ya msingi, dawa zimeshushwa kutoka ngazi ya hospitali za wilaya hadi vituo vya afya, ili kuboresha huduma za mbalimbali zikiwemo zinazohusisha upasuaji.
Na Happiness Mtweve



























