Na Benedict Mwasapi, Dodoma
OFISI ya Taifa ya Mashitaka imefanikiwa kutaifisha zaidi ya sh. bilioni 44, kutoka kwa taasisi zinazohusika kufanya udanganyifu wa kuwatapeli Watanzania kwa kuendesha mchezo haramu wa upatu.
Taasisi hizo zinazodaiwa kuhusika na udanganyifu kwa madai ya kupewa kibali cha uendeshaji kutoka mamlaka za serikali ni Rifaro Africa, IMS, Mr. Kuku, Development Enterpreneurship Initiative (DECI) na QNET Limited.
Mkurugenzi wa Mashitaka, Biswalo Mganga, ametaja fedha ambazo zilitaifishwa kutoka katika kila taasisi na kiwango chake katika mabano ni DECI (sh. bilioni 16), D9 (sh. milioni 500), Rifaro (sh. bilioni 3.4), Mr Kuku (sh. bilioni 5.1) huku taasisi ya IMS ikitaifishwa sh. bilioni 16.
Akizungumza jana, mkoani hapa, Mganga, alisema biashara haramu ya upatu ni kosa la jinai chini ya vifungu namba 171 A, 171 B na 171 C vya Sheria na Kanuni ya Adhabu.
Alisema vitendo hivyo vinakiuka masharti ya Sheria ya Benki na Taasisi za Kifedha ya Mwaka 2006, inayokataza mtu yeyote kupokea miamala ya kifedha kutoka kwenye umma bila leseni.
“Mipango hii imekuwa kama janga kwa wananchi kupoteza fedha zao kutokana na ulaghai wa udanganyifu wa kunufaika kwa haraka baada ya kujiunga na taasisi hizo. Taasisi zinazohusika na udanganyifu huo ni Rifaro Africa, IMS, Mr Kuku, Development Enterpreneurship Initiative (DECI) na QNET Limited,” alieleza.
Aliongeza: “Kwa sasa mipango hiyo imeibuka kwa sura mpya kama biashara ya kimtandao na wananchi wengi wamekuwa wakishiriki, matokeo yake wanadhurumiwa fedha zao, waendeshaji wa mipango hiyo tutahakikisha tunawachukulia hatua kali za kisheria na kutaifisha fedha walizozichukua kwa wananchi.”
Mganga, alisema mbali na kutaifishwa kwa fedha, pia waliweza kubinafsisha mali kama nyumba na magari kutoka katika taasisi hizo.
Alisisitiza kuwa waendeshaji wa mipango hiyo wamekuwa na desturi ya kutumia watu wenye ushawishi kwenye jamii kama viongozi wa kisiasa au dini ili kujenga imani na kuvutia washiriki wapya.
“Taasisi hizi hazina ofisi maalumu zinazotambulika na mara zote wameona ili kuwapata watu, ni vyema kutumia kimvuli cha kutoa misaada kwa jamii husika ili kupenyeza ulaghai wao na mwisho wake kudhulumu mali za wanachama wao,” alisema.
Hivi karibuni, kumekuwa na matukio mengi ya kihalifu yananyotokana na ulaghai wa taasisi za kifedha kwa kuwapatia wananchi manufaa ya haraka, kinyume chake wamekuwa wakitumia njia kuwadhurumu fedha wananchi pindi wakijiunga na taasisi hizo.