WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imetoa kipaumbele cha ajira kwa wenye ulemavu, hivyo amewataka wajitokeze kwa wingi kuomba nafasi za ajira pindi zinapotangazwa.
Majaliwa aliyasema hayo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Stella Ikupa, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake, mbunge huyo aliitaka serikali inapotangaza nafasi za ajira itenge asilimia fulani kwa ajili ya wenye ulemavu tofauti na utaratibu uliopo sasa.
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema serikali imeweka utaratibu maalumu wa uendeshaji wa michakato ya ajira katika Sekretarieti ya Ajira na kutoa upendeleo kwa wenye ulemavu pale zinapotangazwa ajira.
“Hata katika teuzi mbalimbali anazozifanya na Rais Samia, ametoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu.
Hata hivyo watu wenye ulemavu wanapata fursa ya kwanza kwenye usaili wa ajira mbalimbali,” alieleza.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema katika kuhakikisha Bandari za Mtwara na Tanga zinatumika ipasavyo, serikali imeamua kutoa punguzo la asilimia 30 ya tozo katika gharama za kuhudumia shehena na meli kama sehemu ya mikakati ya kimasoko kuvutia wateja kutumia bandari hizo.
Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nanyamba (CCM) Abdallah Chikota, aliyetaka kujua serikali ina mikakati gani kuwavutia wafanyabiashara wa Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kutumia Bandari ya Mtwara na nchi nyingine zikiwemo Sudan Kusini na Uganda kutumia Bandari ya Tanga.
“Serikali kupitia Rais wetu Samia Suluhu Hassan, imetenga fedha kwa ajili ya maboresho ya bandari zetu zote nchini zilizopo ukanda wa bahari kuu na katika maziwa makuu kwa kuimarisha miundombinu mbalimbali.
Aliongeza kuwa: “Tumeongeza vifaa vinavyoweza kupakia na kupakua mizigo kwa muda mfupi, tumepunguza tozo katika Bandari za Tanga na Mtwara ili wateja wanaoleta mizigo katika bandari hizo kuwahakikishia upatikanaji wa huduma kwa muda mfupi zaidi.”
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakabirisha wafanyabiashara wa mafuta kutumia bandari hizo kwani licha ya kupunguza tozo, serikali imefunga mita za kisasa za kupakua na kupakia mafuta kurahisha upakuaji, upakiaji wa shehena hiyo na yamejengwa matenki ya kutosha.
Alisema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatumia balozi za Tanzania kuhamasisha wafanyabiashara kutumia bandari na imefungua ofisi katika nchi za DRC, Malawi na Zambia ili wateja wanaohitaji huduma kupitia bandari hizo watapate mawasiliano wakiwa katika nchi zao bila ya kulazimika kuja Tanzania.
Aliwahakikishia wafanyabiashara hao usalama wao na mizigo yao ambapo aliwataka waendelee kutumia vyema bandari za Tanzania.
Alisema licha ya maboresho hayo, serikali itaendelea kuboresha miundombinu mingine ya usafiri na usafirishaji hususan reli na barabara ili kuunganisha vyema na nchi jirani kwa lengo la kuleta ustawi wa kibiashara na kiuchumi.



























