SERIKALI imetahadharisha kuna visa kadhaa vya Uviko -19 katika jamii, ambavyo vinasambaa haraka, hivyo imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga.
“Bado tupo katika hali nzuri ya Uviko -19, hata hivyo bado Uviko upo katika jamii yetu na mpaka sasa hivi kuna visa kadhaa ndani ya jamii, lakini siyo vingi ni vichache ambavyo vinasambaa kwa haraka kwa hiyo tunatoa tahadhari kwa wananchi waendelee kujikinga.”
Aidha, imelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na wamiliki wa vyombo vya usafiri nchini, kuhakikisha hakuna kusimamisha abiria na kuhimiza uvaaji wa barakoa katika mabasi hususan kipindi hiki ambacho watu wengi wanasafiri kwenda kusherehekea sikukuu.
Hayo yalibainishwa jijini Dodoma Desemba 19, 2021 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa kampeni jamii shirikishi ya pili dhidi ya afua za kinga ya Uviko-19 itakayofanyika jijini Arusha, Desemba 22, mwaka huu.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia matumizi ya chanjo ya Uviko-19 na Julai 23, mwaka huu, kwa mara ya kwanza Tanzania ilianza kutoa chanjo hizo ikianza na Jenssen, baadaye Sinopharm na Pfizer
Profesa Makubi alisema hadi juzi watu milioni 1.27 wamechanja chanjo kamili na kinga dhidi ya Uviko-19 sawa na asilimia 2.21 huku lengo likiwa ni kuhakikisha asilimia 60 ya Watanzania wanachanja. “Lengo la serikali ni kufi kia asilimia 60 ya wananchi wote.
Ili kufanikisha malengo ya awamu ya pili na matumizi ya watoa huduma ngazi ya jamii, Wizara na ORTAMISEMI imeandaa mwongozo wa wawezeshaji wa wahudumu wa afya ya jamii,”alisema.
“Hali ni nzuri, lakini bado Uviko upo kwenye jamii na mpaka sasa tuna visa kadhaa ndani ya jamii, lakini vinasambaa kwa haraka, hivyo wananchi waendelee kujikinga kwa kutumia njia zilizoanishwa na wizara ikiwemo kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kuchanja, kuvaa barakoa na kunawa mikono.
“Inabidi kufanya hivyo kwa sababu hali hiyo inaweza kuleta athari kama vikisambaa hivyo tuendelee kudhibiti ili visiende mbali zaidi na kusababisha madhara makubwa,”alisema Profesa Makubi.
Aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari hususan wanaosafi ri kipindi hiki cha sikukuu ikiwemo Jeshi la Polisi na wamiliki kuhakikisha wanadhibiti kujaa mabasi kwa kutoa elimu na si nguvu.
“Pia wahakikishe wananchi hawajai katika daladala, lakini wasitumie nguvu wawaelimishe kuhusu athari za ugonjwa huu, pia wanafunzi waliopo likizo waepushwe na misongamano isiyo ya lazima, wavalishwe barakoa na kunawa mikono,”alisema.
Profesa Makubi aliongeza kuwa: “Wanaosafi ri kwenda kutembelea wazazi, wazee mikoa mbalimbali nchini kipindi hiki hakikisheni mnachukua tahadhari ili kuwakinga hasa wale wenye magonjwa ya muda mrefu,”.
Vilevile, aliwataka watu ambao wamechoma chanjo kurudia mara ya pili kwa kuwa mfumo umewekwa wa kuwatumia ujumbe wanaotakiwa kufanya hivyo na hata waliohama mkoa, mfumo utawawezesha kuchoma katika maeneo waliopo.
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa kampeni hiyo, Profesa Makubi alisema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na wizara zingine, wanatarajia kuzindua kampeni ya utekelezaji wa Mpango Shirikishi na Harakishi Awamu ya Pili dhidi ya UVIKO-19 nchini Tanzania, itakayofanyika jijini Arusha.
Alibainisha katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Manyara, Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Kilimanjaro, Geita, Ruvuma na Morogoro tayari wahudumu zaidi ya 8,130 wamepatiwa mafunzo na wanaendelea na kazi ya uhamasishaji huku zoezi hili likiwa ni endelevu katika maeneo mengine nchi nzima.
Profesa Makubi alisema katika mpango huo zinaelekezwa timu za afya katika halmashauri na mikoa kuendelea kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii, ili kuendelea kuhamasisha na kuelimisha juu ya hatua mbalimbali za kujikinga na UVIKO – 19 ikiwa ni pamoja matumizi ya chanjo.
Alieleza lengo la serikali ni kushirikiana na wananchi wenyewe na wadau wa maendeleo kuongeza chachu kwa watoa huduma ngazi ya jamii kuendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii kuendelea kuchukua tahadhari.
Alifafanua kupitia kampeni hiyo mambo yatakayozingatiwa ni kuwezesha serikali za mitaa, vitongoji kusimamia zoezi hilo la elimu na utoaji wa chanjo na liwe endelevu (Kampeni ya Mtaa kwa Mtaa na Kitongoji kwa Kitongoji).
Aidha, kuendelea kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ili waendelee kutoa huduma ya chanjo kulingana na miongozo ya nchi na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Nyingine ni waganga wakuu wa mikoa na halmashauri kuongeza vituo vya kutolea huduma za chanjo kulingana na mahitaji, zikiwemo huduma mkoba na kufungua vituo zaidi katika maeneo ya mikusanyiko.
Pia, kuzitaka halmashauri kuendelea kuwajengea uwezo kata, vijiji na vitongoji katika kuelimisha jamii na kupeleka huduma za chanjo kwenye jamii.
“Vilevile, kuendelea kuwatumia watu maarufu kama viongozi wa dini, wasanii, wanasiasa, wana jamii, wana nzengo, wanahabari na viongozi/wazee wa kimila katika mapambano dhidi ya Uviko – 19,”alisema Profesa Makubi.
Na SELINA MATHEW, Dodoma



























