Na HANIFA RAMADHANI Na EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imetoa muda wa mwezi mmoja kwa wakandarasi wa ujenzi wa miradi ya miundombinu ya umwagiliaji maji ya kilimo kwa ajili ya vijana kuhakikisha wanamaliza kazi zilizobakia.
Miradi hiyo ni ule wa Chia Bonde Makunduchi, Koani na Chuo cha Amali Makunduchi.
Pia, imeonya uongozi wa wakandarasi hao, ambao ni Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) na Kampuni ya Main, kuwa serikali ya awamu ya nane haitasita kuwawajibisha endapo muda huo wa uliotolewa hautatekelezwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, alipofanya ziara ya kutembelea wilaya zote za Unguja na Pemba, kuangalia maendeleo na changamoto zinazozikabili wilaya hizo.
Alisema serikali imejikita kuendelea kuimarisha miundombinu ya kuwawezesha vijana kuwa na nguvu za kujitegemea kiuchumi, hivyo haitapendeza kuona wapo watu na baadhi ya taasisi zinachangia kuzorotesha miradi husika.
Makamu huyo wa Pili wa Rais, aliagiza serikali ya mkoa wa Kusini Unguja, kwa kushirikiana na watendaji wake waandamizi, kuifuatilia kwa karibu miradi hiyo ili kujiridhisha na hatimaye kuhakikisha inamalizika kama alivyoagiza.
Alisema serikali inaendelea na utekelezaji wa ahadi zake iliyozitoa wakati wa kuomba ridhaa ya kuongoza serikali, hususan suala la ajira kwa vijana, ili kuona Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025, inatekelezeka kwa kuwapatia vijana ajira 300,000, katika kipindi cha miaka mitano.
“Ifikapo mwaka 2025, maswali na changamoto zilizokuwa zikiwasumbua wananchi, zitabakia kuwa historia na CCM tayari itakuwa imeshakidhi kiu iliyokuwa nayo kwa Wanzanzibari,” alisema.
Mwanajuma Khamis Makame, mkazi wa Kijiji cha Muyuni, alielezea changamoto za kijiji hicho, ikiwemo migogoro ya ardhi, ambapo alimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kutatua tatizo hilo ambalo limekuwa sugu.
Alisema kuna haja ya kulitafutia ufumbuzi suala hilo, ambapo serikali ya wilaya na CCM mkoa wa Kusini Unguja, zinapaswa kukaa pamoja na kulitafutia ufumbuzi kwani limekuwa sugu kwa muda mrefu.