Na SYLVIA SEBASTIAN
SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne (jina linahifadhiwa), amedai alimkuta mtoto wake gengeni akiwa amevuliwa suruali hadi chini ya magoti huku ameinamishwa kisha ameingiziwa uume kwenye haja kubwa.
Shahidi huyo, ambaye ni mlinzi na baba mzazi wa mtoto huyo (majina tunayahifadhi), amedai hayo katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, mbele ya Hakimu Mkazi, Anna Mpessa, wakati shauri hilo linalomkabili Shaibu Kibunda, lilipopelekwa kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi upande wa Jamhuri.
Amedai Septemba 20, mwaka jana, saa 5 asubuhi, alirudi nyumbani kwake akitokea kazini, ambapo baada ya kufika, alimkuta mkewe na kumuuliza alipo mtoto wakati huo na kujibiwa yupo kwa Shaibu gengeni.
Shahidi huyo alidai baada ya kupewa majibu hayo, alikwenda kumuangalia gengeni kwa Shaibu, ambako alimkuta mtoto huyo ameinamishwa akiwa ameshikilia kwenye tenga, akiwa amevuliwa suruali yake hadi chini ya magoti.
Alidai baada ya kukuta hali hiyo, alimuuliza mshtakiwa kwa jazba kwa nini anamlawiti mtoto wake, ndipo alishtuka, akatoa uume wake kwenye eneo la haja kubwa ya mtoto kisha akampandisha suruali.
“Nilizunguka nyuma ya genge na alivyoona nataka kuingia, aliinua sahani yake ya wali iliyokuwa kwenye boksi. Kabla ya kuishika hiyo sahani, nilimfuata, nikampiga vibao vitatu, akaomba msamaha.
“Nilimwambia siwezi kukusamehe na wakati huo mke wangu alifika na kuuliza kilichotokea, nikamwambia nimemkuta anamlawiti, mchukue mtoto nenda naye nyumbani, lakini asimuogeshe,” alidai.
Alidai baada ya kutoa maelekezo hayo, alikwenda nyumbani kwa walezi wa kijana huyo, ambao ni mjomba wake na shangazi na kuwaeleza hali hiyo.
Shahidi huyo alidai baada ya kuwapa taarifa hizo, walionyesha hali ya huzuni huku shangazi yake akadai kwamba, ikibainika amefanya kweli, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela, kwani kitendo hicho kinauma.
“Nilirudi nyumbani nikamwambia mke wangu amlaze mtoto kwenye kochi, nikamwangalia sehemu ya haja kubwa, kulikuwa na damu, ambayo ilikuwa imechanganyika na rangi nyeupe, nikasema bila shaka hizi ni shahawa.
“Baada ya kuona hali hiyo, nilirudi kwa mjomba wa kijana huyo, nikawaeleza namuhitaji huyo kijana kwenda naye hospital pamoja na mtoto wangu, mjomba wake akadai twende pamoja Hospitali ya Zakheem,” alidai,
Shahidi huyo alidai baada ya kufika hospitalini, walidai kwamba hawawezi kuonana na daktari hadi wawe na fomu namba tatu (PF3), hivyo wanatakiwa wakaichukue.
“Tuliondoka wote hadi kituo cha polisi Kizuiani na baada ya kufika kituoni hapo, niliwasimulia tukio hilo, wakadai mtuhumiwa hawawezi kurudi naye hospitali, watabaki naye, hivyo nikaondoka na mjomba wa mtuhumiwa hadi hospitali, kisha kujiandikisha kwa ajili ya kusubiri huduma,” alidai.
Mkata, alidai wakati wanaendelea kusubiri kupewa huduma kutokana na foleni kuwa kubwa na muda unazidi kwenda, mtoto huyo alimwambia baba yake anajisikia kwenda kujisaidia haja kubwa.
“Ilibidi nimfuate nesi kumuelezea kwamba huyo mtoto amelawitiwa na anataka kwenda haja kubwa, akanielekeza niende chumba namba saba, nitamkuta daktari, nikamueleza, akaniambia nisubiri kidogo na muda mfupi alianza kumuhudumia mtoto,” alidai.
Alidai baada ya kumueleza daktari, alimwambia ampandishe mtoto juu ya kitanda kisha amvue nguo ashikilie kitanda na kuinama ili amchunguze haja kubwa.
“Daktari aliachanisha sehemu ya haja kubwa, akamuingizia kidole, làkini hakushtuka. Daktari aliandika kwenye daftari ili akachukuliwe vipimo maabara na wakati tuko maabara, daktari alidai muda wake umekwisha, hivyo atajaza majibu siku iliyofuata,” alidai
Shahidi huyo alidai baada ya kipimo hicho, kilihitajiwa kipimo kingine, akaambiwa akapimwe na daktari, ambaye alikuwa ameingia zamu wakati huo, akampima.
“Wakati mtoto anapimwa vipimo vyote viwili, nilikuwa naangalia pamoja na mjomba wake, kipimo cha pili alivyopimwa na daktari, alimuingiza kifaa kwenye haja kubwa na alivyokitoa, kilitoka na damu kisha nilipewa nipeleke maabara. Kwa kuwa yule daktari wa awali alikuwa ameshaondoka, yule mwingine alidai hawezi kujaza hadi yule wa mwanzo.
“Ilibidi turudi polisi kuwaeleza kwamba PF3 hadi kesho yake, polisi walidai hawezi kukaa na mtuhumiwa, labda tutarudi naye kesho, nikawaambia namfungulia kesi ya kulawiti,” alidai.
Shahidi huyo alidai kesho yake, alikwenda kufuatilia hayo majibu,
daktari akamueleza kwamba mtoto aliingiliwa na kipimo kilionyesha damu.
Hakimu Anna, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 25, mwaka huu na mshitakiwa yuko nje kwa dhamana
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, inadaiwa Septemba 20, mwaka jana, eneo la Mbagala Goroba B, Temeke,
Dar es Salaam, Kibunda (24) alimlawiti mtoto wa miaka minne (jina linahifadhiwa)