KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kubana mianya ya upotevu wa mapato mkoani Kigoma ikiwemo kuwabana baadhi ya wafanyabiashara wakubwa.
Shaka amesema zipo taarifa za upotevu wa zaidi ya sh. bilioni mbili kila mwaka mkoani humo, huku baadhi ya wafanyabiashara na watumishi wa umma wakitajwa kuwa vinara katika kuikosesha mapato serikali.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki akiwa katika ziara ya Sekretarieti ya CCM, kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na uimara wa Chama mashinani, ambapo alitembelea Bandari na Stesheni ya Reli Kigoma.
“Nikupongeze meneja mpya wa TRA (Gabriel Mwangosi) kwa kuletwa hapa Kigoma, ni matumaini yangu kwamba rai hii, ambayo tumeitoa utaanza nayo kuifanyia kazi, nina taarifa kuwa umeanza vizuri hongera… endelea kusimama vizuri.
“Zaidi ya sh. bilioni mbili kwa mwezi zinapotea kwenye ukusanyaji wa ushuru wa forodha (Kigoma), hili halipo sawa,” alisema.
Shaka aliitaka TRA na serikali kwa ujumla kujiuliza fedha zinazopotea zinakwenda wapi, huku makusanyo ya mwezi katika mkoa huo yakiwa sh. milioni 700.
“Wapo wafanyabiashara ambao wanajulikana, yupo ambaye ni wa kati, kazi yake ni kuchezesha ili kuona mapato ya katikati yanakwenda kwake na unao wafanyakazi ambao si waaminifu wanashirikiana kuhujumu mapato ya serikali,” alisema Shaka.
Kadhalika alisema fedha hizo zikiingia katika mfuko wa serikali, zitasaidia kuubadilisha mkoa wa Kigoma kiuchumi na kutatua changamoto zinazowakabili.
Shaka alimtaka Mwangosi kuhakikisha anaziba mianya ya upotevu wa mapato ya serikali na pasiwepo na watu wachache ambao wanaihujumu.
Katibu huyo wa NEC alisema ana taarifa kuwa TRA katika mkoa huo inakabiliwa na changamoto ya wafanyakazi na vitendea kazi yakiwemo magari, hivyo ni vyema kuhakikisha mianya inayosababisha upotevu wa sh. bilioni mbili inazibwa ili zifanikishe kuongeza ufanisi.
Aliongezea kuwa: “Mimi ninaamini kuletwa kwako hapakuwa kwa bahati mbaya tumefuatilia huko ulikotoka ulifanya vizuri na hapa tuna matumaini kwamba utakuja kubadilisha hizi changamoto zilizokuwa katika huu mkoa wa Kigoma, sisi kwa miaka mitano tumeahidi kuijenga nchi hii.”
Akizungumza kuhusu usafiri wa treni, Shaka alisema Chama kitaendelea kuisimamia serikali kuhakikisha unaendelea kuboreshwa ili uendelee kuwa mkombozi kwa wananchi wa mkoa huo.
Pia aliwataka watumishi wanaopewa dhamana kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na ufikishaji huduma kwa wananchi.
Na MWANDISHI WETU, Kigoma



























