KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ameeleza kusikitishwa kutokana na kuongezeka kwa ujauzito na utoro kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.
Pia, ameshangazwa na hatua ya halmashauri hiyo kujiwekea utaratibu wa kuwatoza faini ya sh. 245,000 na mifuko 10 ya saruji wazazi wenye watoto waliopata ujauzito.
Hayo aliyasema wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na Sekretarieti ya Chama wilayani humo.
Ametoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Vincent Anney, kusitisha uamuzi huo na kurejesha fedha zote walizowatoza wazazi wenye watoto waliopata ujauzito, huku akisisitiza sheria kuchukua mkondo wake dhidi ya watuhumiwa.
“Hatuwezi kukomesha vitendo hivi kwa kutozana faini, kisha yaani mtu mwanaye anapewa mimba anatozwa faini kisha yeye na mhalifu wote wanabaki uraiani,” amesema Shaka
Ametolea mfano tukio moja linalomuhusisha mjane mwenye umri wa miaka 67, ambaye ametozwa faini ya sh. 245,000 na mifuko 10 ya saruji kwa kuwa mwanaye amepewa ujauzito, huku Mkurugenzi wa Halmashauri akiwa amefumbia macho hilo.
Alibainisha kitendo hicho ni kubadili maudhui na kuzitafsiri vibaya sheria za nchi.
“Mkuu wa Wilaya sitisha utekelezaji wa uamuzi huu kwa shule zote na fedha zote zilizokusanywa zirejeshwe kwa wahusika na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zichukuliwe kwa waliohusika na tupewe mrejesho ndani ya siku saba,” aliagiza.
Aidha, alifafnua kuwa CCM na serikali haitavumilia vitendo vya rushwa katika kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo hawataruhusu watendaji wasiyo waadilifu wakigombanishe Chama na wananchi. Aliwataka watendaji wa serikali wanapofanya ziara za kikazi kufika vijijini, kwa kuwa kuna shida kubwa na hivyo wasiridhike na taarifa wanazopokea.
“Waliopewa dhamana lazima mtafisiri kwa usahihi sheria za nchi ili kumaliza kero kwa wananchi. Jamii iwalinde watoto ili wakue katika malezi mazuri na kupata elimu waje kutumikia nchi yao,” alisema.
Katika ziara hiyo wananchi walilalamikia utaratibu wa kulazimishwa kununua mbolea katika maduka ya pembejeo ya Maofisa Ugani ndipo wapewe iliyotokana na ruzuku ya serikali, na kwamba bila ya kufanya hivyo hawapati. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, wanaendelea na ziara ya kikazi mkoani Mbeya.
Na MWANDISHI WETU